Robert Card ambaye maafisa wa usalama wa Marekani wanaamini alihusika kwenye mauaji hayo, alipatikana akiwa amekufa Ijumaa jioni, karibu na eneo ambapo alikuwa anafanya kazi kwa wakati mmoja. Polisi walisema Card aliacha ujumbe kabla ya kifo chake, lakini hawakutoa maelezo Zaidi.
Michael Sauschuk ambaye ni kamishna wa usalama wa umma jimboni humo wakati akihutubia wanahabari Ijumaa amesema kwamba huenda Card alikufa kutokana na kujipiga risasi mwenyewe. Gavana wa jimbo hilo Janet Mills amesema kwamba mwili wa Card ulipatikana karibu na mji wa Lisbon Falls. Mamlaka zimekuwa zikimsaka Card kufuatia mauaji ya halaiki Jumatano kwenye maeneo mawili mjini Lewiston, Maine.
Anashukiwa kuuwa watu 18 kwa kuwapiga risasi, huku akijeruhi wengine 13, wakiwemo wanne ambao ni viziwi. Kupitia taarifa ya Alhamisi, Rais Joe Biden alisifu maafisa wa usalama kwa juhudi zao za kumsaka mshukiwa huyo, wakati akiomba wabunge wasaidie katika kuunda sheria za kupunguza uhalifu wa bunduki.
Kiujumla Wademokrat wanaunga mkono sheria hizo wakati wa Repablikan wakisema kwamba zinahujumu marekebisho ya pili ya katiba, yanayoruhusu wamarekani kumiliki silaha kwa ajili ya kujilinda.
Forum