Rais wa Guinea, Alpha Conde, amepata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo na kupata kupata awamu ya tatu madarakani.
Matokeo kutoka wilaya 37 kati ya 38 yanaonyesha kwamba Conde amepata kura nyingi, mara mbili zaidi ya mshindani wake wa karibu Cellou Dalein Diallo, ambaye amesema ana ushaidi wa kutosha kwamba udanganyifu mkubwa ulifanyika katika hesabu ya kura na kwamba atawasilisha kesi katika mahakama ya kikatiba.
Conde, mwenye umri wa miaka 82, amepata zaidi ya kura milioni 2.4 ikilinganishwa na kura milioni 1.2 za Cellou Dalein Diallo.
Maandamano yanaendelea nchini humo na watu 13 wanaripotiwa kuuawa tangu Jumapili, siku upigaji kura ulipofanyika.
Diallo amejitangaza mshindi wa uchaguzi huo.
Conde atoa wito wa utulivu
Rais Conde ametoa wito kwa raia wote wa Guinea kuwa watulivu licha ya makabiliano mabaya kati ya wafuasi wa upinzani na polisi kuongezeka.
“Nasisitiza ombi langu kwa raia wote wa Guinea kuwa watulivu wakati tunasubiri mchakazi wa uchaguzi kumalizika,” amesema rais Conde, akiongeza kwamba “kama ushindi ni wangu, nitakaribisha mazungumzo na nipo tayari kufanya kazi na watu wote wa Guinea.”
Waziri wa usalama Damantang Albert, amesema kwamba watu sita wamekufa, wakiwemo maafisa wa polisi wawili na wengine kadhaa kujeruhiwa katika makabiliano katika ngome za upinzani nje ya mji wa Conarkry.
Guinea imekuwa katika mgogoro wa kisiasa kufuatia hatua ya rais Alpha Conde kugombea muhula wa tatu madarakani baada ya kubadilisha katiba.
Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC