Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Mei 08, 2024 Local time: 23:56

Ghana yashinda na kuingia robo fainali


Ghana timu pekee ya Afrika iliyobaki kwenye michuano ya kombe la dunia yafanikiwa kuingia robo fainali.

Ghana imekua timu pekee ya Afrika iliyofanikiwa kuingia katika robo fainali ya michuano ya kombe la dunia baada ya kuibwaga Marekani mabao 2-1 katika muda wa ziada na kuweka historia ya kuwa nchi ya tatu katika Afrika kufika hatua ya robo fainali.

Ilikuwa ni Ghana iliyokuwa ya kwanza kuuona mlango wa Marekani kupitia kwa Kevin Prince Boateng aliyepiga shuti kali la chini lililomshinda mlinda mlango wa Marekani Tim Howard na kupata kukalia usukani wa pambano hilo mapema. Lakini Marekani walipambana kufa na kupona mpaka mapumziko bado Ghana walikuwa wakiongoza.

Kipindi cha pili Marekani walifanya mabadiliko na kuongeza mashambulizi na hatimaye yalizaa matunda baada ya Clint Dempsey kuangushwa kwenye eneo la hatari ambapo walipata penalti iliyowekwa kimiani na mshambuliaji hatari wa Marekani na LA Galaxy Landon Donovan.

Mpaka mwisho wa dakika 90 timu ya Marekani pamoja na kukosa nafasi kadhaa ilishindwa kupata bao la ushindi kwani ukuta wa Ghana ukiongozwa na kipa wao mahiri Richard Kingson uliweza kuzuia hatari langoni mwao.

Katika muda wa ziada ilikuwa ni Ghana waliotumia vizuri nafasi waliyoipata mapema katika dakika ya tatu tu mchezaji hatari Asamoah Gyan alipachika bao la pili na la ushindi.

Hadi mwisho wa muda wa ziada walikuwa ni Ghana waliotoka kifua mbele baada ya Marekani kushindwa kupata bao la kusawazisha sasa Ghana watakumbana na Uruguay ambao walikuwa wa kwanza kuingia robo fainali siku ya Jumamosi.

Na katika hiyo mechi ya kwanza Jumamosi Uruguay ilipata tiketi ya kucheza robo fainali hizo baada ya kuwafunga Korea Kusini mabao 2-1, mabao yote ya Uruguay yalifungwa na Luis Suarez na bao la Korea Kusini lilifungwa na Lee Chung Yong kunako daika ya 69 ya mchezo huo.

Michezo mingine ya raundi ya pili inaendelea Jumapili ambapo katika mchezo wa kwanza siku Uingereza watapambana na Ujerumani na katika mchezo huu wa kihistoria kocha wa Uingereza Fabio Capello amesema mshambuliaji wake hatari Wayne Rooney yuko tayari kwa mpambano huo na amefunga magoli mengi mazoezini akitegemea ataweza kufanya hivyo kwenye mechi yao.

Na mchezo wa pili utakuwa ni kati ya Argentina na Mexico huko Johanesburg. Katika michezo mingine ya raundi ya pili Brazil watakumbana na Chile, Ureno watacheza na Hispania nao Uholanzi watapambana na Slovakia wakati Paraguay wataonyeshana kazi na Japan.

XS
SM
MD
LG