Makundi hayo yameiomba serikali ya Rais Adama Barrow kutafuta msaada wa nchi za Afrika magharibi kumrudisha Jammeh kutoka uhamishoni nchini Guinea Equatorial na kumfungulia mashtaka.
“Tuna wasiwasi kwamba Rais Barrow alifanya ziara Guinea Equatorial lakini hakuweza hata kuzungumzia suala la kurudishwa kwa Jammeh,” makundi hayo yamesema katika taarifa.
Barrow alishiriki mkutano wa Umoja wa Afrika uliofanyika Guinea Equatorial, kuanzia tarehe 25 hadi tarehe 28 Mei. Baada ya mkutano huo, alibaki huko kwa ziara ya kikazi ya siku mbili, msemaji wa rais Ebrima Sankareh aliiambia AFP.
Sankareh alisema suala la Jammeh lilizungumziwa kidogo wakati wa mazungumzo kati ya Barrow na Rais wa Guinea Equatorial Teodoro Obiang Nguema, lakini nchi hizo mbili zilikubaliana kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na kushirikiana kwenye sekta ya mahakama na masuala mengine.
Ziara hiyo ilijiri siku chache baada ya waziri wa sheria wa Gambia kukubali mapendekezo mengi ya tume ya ukweli, ambayo iliendesha uchunguzi kuhusu madai ya manyanyaso yaliyofanywa na Jammeh na maafisa wengine wa serikali wakati wa utawala wake wa miaka 22.