Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 08, 2022 Local time: 14:58

Burundi: Ndayishimiye ndiye mshindi wa urais, Mahakama yaamua


Evariste Ndayishimiye.

Mahakama ya katiba nchini Burundi Alhamisi iliidhinisha matokeo ya uchaguzi wa Mei 20 mwaka huu kama yalivyotangazwa na tume ya uchaguzi ya nchi hiyo.

Hiyo inamaanisha kwamba Évariste Ndayishimiye ndiye mshindi wa uchaguzi wa urais baada ya kupata asili mia 67 ya kura zote zilizopigwa.

Katika uamzi huo, mahakama hiyo ilisema kuwa malalamishi ya mgombea kiti cha urais kwa niaba ya chama cha upinzani, Agathon Rwasa, na yale ya kanisa Katoliki wakidai kuwa uchaguzi huo uligubikwa na wizi wa kura na udanganyifu mwingi, hayana msingi.

Hayo yalijiri baada Rwasa, ambaye pia ndiye kiongozi wa chama cha upinzani, CNL, kuwasilisha hoja zake kwenye mahakama hiyo, akidai uchaguzi uligubikwa na dosari nyingi, zikiwa ni pamoja na wizi wa kura.

Kulingana na katiba ya Burundi, uamuzi wa mahakama ya katiba hauna rufaa.

Agathon Rwasa
Agathon Rwasa

Hata hivyo, awali, Rwasa alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kwamba iwapo hatapata haki kwenye mahakama ya katiba, atawasilisha malalamishi yake kwa mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa tume ya uchaguzi ya Burundi, Rwasa alipata asili mia 22.42.

Hafla ya kuapishwa kwa Ndayishimiye kama rais itafanyika tarehe 26 mwezi Agosti, ambapo pia ataanza muhula wa miaka 7, kulingana na Katiba ya Burundi.

-Imetayarishwa na Patrick Nduwimana, VOA, Washington DC.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG