Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Februari 09, 2023 Local time: 05:39

Ethiopia yasema ipo tayari kwa mazungumzo na TPLF bila masharti


Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed

Katika  hatua isiyo ya kawaida, afisa mmoja wa ngazi ya juu kwenye serikali ya Ethiopia amesema Alhamisi kwamba wako tayari kwa mazungumzo na vikosi hasimu vya  TPLF, vilivyoko kaskazini mwa nchi, wakati wowote , mahala popote na bila ya masharti. 

Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, matamshi hayo yametolewa na Redwan Hussein mshauri wa usalama wa waziri mkuu Abiy Ahmed, wakati kukiwa na matumiani ya kuwepo majadiliano ya kusuluhisha mapigano yaliyozuka hapo Novemba 2020.

Redwan alitweet baada ya mkutano na wawakilishi maalum kutoka Umoja wa mataifa , Umoja wa Ulaya na Marekani, akiongezea kwamba Umoja wa Afrika utaongoza mchakato huo, na kwamba unaweza kuomba msaada wa kiufundi kutoka kokote.

Baada ya sitisho la mapigano la Juni, pamoja na kuruhusiwa upelekaji wa misaada kwenye eneo la Tigray, pande zote mbili zilikubaliana kufanya mazungumzo. Serikali kuu ya Ethiopia iliteua wapatanishi 7 wakiongozwa na waziri wa mambo ya nje ingawa upande wa Tigray unasema ni lazima masharti kadhaa yatimizwe kabla ya mazungumzo hayo kufanyika.

Mapema wiki hii, kiongozi wa serikali ya kieneo ya Tigray Debretsion Gebremichael alisema kwamba iwapo serikali kuu ina azma ya kweli ya kurejesha amani, basi ingeanza kwa kurejesha huduma za msingi katika mkoa huo kama vile umeme, mawasiliano ya simu na benki.

Wakosoaji wanasema kwamba hatua inayohitajika ni kuondolewa kwa viongozi wa Tigary pamoja na kupokonywa silaha kwa wapiganaji wao, kabla ya mazungumzo kuanza. Baadhi wanasema pia kwamba itakuwa kinyume cha sheria kwa serikali kufanya mashauriano na TPLF wakati bado liko kwenye orodha ya serikali ya Ethiopia ya makundi ya kigaidi.

Serikali ya Ethiopia imekuwa katika shinikizo la kimataifa kufanya mashauriano na viongozi wa Tigray, ili kumaliza mapigano ambayo yameua maelfu ya watu kwenye eneo hilo pamoja na mikoa jirani ya Amhara na Afar.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG