Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Julai 14, 2024 Local time: 22:37

Maandamano zaidi yaendelea huko Cairo


Rais wa Misri Hosni Mubarak akiwa kwenye mkutano mjini Cairo, Jan 30, 2011
Rais wa Misri Hosni Mubarak akiwa kwenye mkutano mjini Cairo, Jan 30, 2011

Maelfu ya raia wa Misri wanaandamana huko Cairo, eneo la Tahrir Square Jumatatu, na kukaidi amri ya kutotoka nje iliyowekwa na serikali, huku wakiendelea kushinikiza kumalizika kwa miaka 30 ya utawala wa Rais Hosni Mubarak.

Helikopta zilipaa juu huku waandamanaji wakitoa wito wa maelfu zaidi kuandamana mjini Cairo Jumanne, kumshinikiza Mubarak ajiuzulu. Pia wametoa wito wa mgomo wa pamoja, licha ya kuwa tayari mji mkuu wa Cairo umefungwa.

Vyombo vya habari vya Misri vinasema Rais Mubarak amemteuwa waziri mpya wa mambo ya ndani na waziri wa fedha katika kile wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema ni jaribio la wazi la kuwanyamazisha waandamanaji wenye hasira. Waziri wa mambo ya nje na waziri wa ulinzi wa muda mrefu waliendelea kushikilia nafasi zao katika baraza la mawaziri lililofanyiwa marekebisho.

Ripoti kutoka Cairo zinasema mkurugenzi wa zamani wa magereza, Jenerali Mahmoud Wagdy atachukua nafasi ya Habib Adly kama waziri wa mambo ya ndani, ambaye analiangalia jeshi la polisi na majeshi ya ulinzi wa ndani. Raia wengi wa Misri walitoa wito wa kutaka afukuzwe kazi baada ya mapigano yaliyosababisha vifo wiki iliyopita kati ya polisi na waandamanaji.

Polisi walirudi mitaani Jumatatu, lakini vyanzo vya usalama vinasema wamepewa amri ya kufanya kazi za kawaida za polisi bila kutumia nguvu za aina yeyote za kuwabughudhi waandamanaji.

Maelfu ya watalii wamerundikana kwenye viwanja vya ndege vya Misri katika juhudi za kukimbia ghasia hizo. Mataifa kadhaa yameshapeleka ndege za kuwachukua raia wao kutoka Cairo. Zaidi ya watu 100 wamekufa tangu ghasia za maandamano zilipoanza nchini Misri Jumanne iliyopita.


XS
SM
MD
LG