Desemba Mosi ni maadhimisho rasmi ya siku ya ukimwi duniani. Mataifa mbalimbali yametoa wito wa kukabiliana na ugonjwa huu na hatimaye kuhakikisha unatokomezwa kabisa.
Nchini tanzania mkurugenzi wa shirika linaloshughulika na afya ya mama na mtoto CSI, Stella Mpanda ametoa wito kwa kina mama ambao ndio waathirika wakubwa kuhakikisha wanazingatia afya zao ili wasiambukizwe.
Wakati huo huo Shirika la afya duniani linaadhimisha siku ya Ukimwi duniani Jumanne kwa kusisitiza umuhimu wa kuongeza matibabu ya antiretroviral kwa wale wote wanaoishi na virusi vya HIV.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linasema kiasi cha watu milioni 16 kati ya milioni 37 wanaoishi na HIV, vijidudu vinavyosababisha UKIMWI wanatumia mchanganyiko wa dawa ya ARV na kwamba matumizi ya wale wote wanaoishi na vijidudu hivyo ndio njia pekee yanayoweza kutokomeza janga hilo katika kipindi cha kizazi kimoja.
WHO imekariri uchunguzi mbali mbali unaonyesha kwamba wale ambao wanaanza matibabu mara moja baada ya kuambukizwa ni mara chache sana kuambukiza wengine huku wao wakiishi na afya nzuri.