Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 07, 2022 Local time: 20:19

Hussein Mwinyi, mwanasiasa msiri na mkimya


Dkt Hussein Mwinyi

Jibu la haraka ambalo unaweza kulipata, kumuelezea Dr Hussein Ali Mwinyi, ni kwamba ni mwanasiasa msiri, mkimya, na ambaye huwepo kama vile hayupo.

Chama cha Mapinduzi – CCM – Julai 10 mwaka huu 2020, kilimchagua waziri wa ulinzi wa Tanzania, Dr Hussein Ali Mwinyi, kuwa mgombea urais wa Zanzibar, na kuwashinda wagombea 31 waliojitokeza kuwania nafasi hiyo kubwa zaidi katika serekali ya mapinduzi Zanzibar.

Mwinyi anaingia katika kinyang’anyiro cha urais Zanzibar huku akiwa na jina kubwa. Baba yake, Ali Hassan Mwinyi, ni rais wa zamani wa Zanzibar, na Tanzania. Historia yake ya kisiasa inaanzia mwaka 2000 kwa kugombea ubunge jimbo la Mkuranga, mkoa wa Pwani, baada ya kuitumikia sekta ya afya katika njia utabibu na ukufunzi katika sekta binafsi na serekalini. Mpaka anafikia uteuzi wa kugombea urais wa Zanzibar, Dr Mwinyi amekuwa waziri katika wizara mbalimbali, lakini licha ya yote hayo, Majjid Mjengwa, mwanahabari na mchambuzi wa siasa za Tanzania anasema Dr Mwinyi ni mwanasiasa wa namna hii.

“Ni mwanasiasa ambaye si wa kawaida kama ilivyozoeleka. Hana makeke na si mtu wa kujikweza. Labda hii inatokana na historia yake ya kuwa mtoto wa kiongozi kwa muda mrefu. Mara kadhaa ameonekana ni mtu wa kawaida, utatambua tu kwa vile gari yake ina namba za waziri. Wazanzibari wanapenda watu wasio jikweza na wenye kujiweka kama raia yoyote wa kawaida. Hilo linaweza likamfanya akapata kukubalika na ikizingatiwa anaonekana ni mtu mnyenyekevu tofauti na wanasiasa wengi vijana. Katika miaka yake 53, na hitoria yake huoni ni wapi alikuwa na kelele za kisiasa.” Alisema Majid Mjengwa

Ukimya wake, kidogo umemuweka mbali kidogo na jicho la umma ambalo huona kwa ukaribu haiba na wasifu wa wanasiasa. Akiwa na umri wa miaka 53 kwa sasa, Dr Mwinyi amehudumu kama naibu waziri wa Afya, waziri wa nchi Muungano, wizara ya afya na ustawi wa jamii, na wizara ya ulinzi ambayo anahudumu mpaka sasa, akiwa pia mbunge wa jimbo la Kwahani, Zanzibar. Wachambuzi wengi wanaeleza muda wa miaka 9 aliohudumu kama waziri wa ulinzi umemfanya kuwa mwanasiasa mkimya.

MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi Mhe.Dkt. Hussein Mwinyi akiwahutubia Wanachama wa CCM na Wananchi Pemba katikia uwanja wa Kibirinzi chakechake wakati wa mkutano wake wa kutambulishwa kwa Wananchi uliofanyika leo katika uwanja huo.(Picha na Ikulu)
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi Mhe.Dkt. Hussein Mwinyi akiwahutubia Wanachama wa CCM na Wananchi Pemba katikia uwanja wa Kibirinzi chakechake wakati wa mkutano wake wa kutambulishwa kwa Wananchi uliofanyika leo katika uwanja huo.(Picha na Ikulu)

Akihojiwa na wanahabari wa Mwananchi Communications ya Tanzania, kutaka kuufahamu undani wake, suala la ukimya wake liliibuka, na kikubwa ni kufahamu kwa nini yeye, pengine ni waziri mkimya zaidi, je yeye anapenda usiri?

“Katika wizara ya ulinzi, kwa kiwango kikubwa si sahihi kuweka maisha yetu hadharani. Tunashughulika na masuala yetu kwa usiri.” Alisema Dr Hussein Mwinyi.

Vilevile, katika mahojiano hayo aliweka wazi kwamba yeye ni mtu wa kifamilia zaidi.

“Dr Mwinyi ni mtu wa familia. Mimi ni mume, na baba. Ni mtu ambaye maisha yangu yote yamejikita kwenye desturi za kifamilia, na nina hakika nitaendelea kuwa hivi hata kama nitachaguliwa kuwa rais.”

Amemtaja mke wake kama nguzo muhimu kwake, licha ya kwamba hakufahamika kwenye jamii ya Watanzania kabla ya kuteuliwa kuwa mgombea wa CCM kwa urais wa Zanzibar. Akimuelezea mkewe, Dr Mwinyi anasema.

“Nina shukuru mungu kwa sababu kama wote tunatumia muda mwingi nje ya familia, watoto wetu wasingepata malezi ya wazazi na upendo wanaoupata kutoka kwa mke wangu.”

Licha ya kukiri katika nyakati tofauti kwamba mchakato wa uteuzi wake ndani ya chama chake cha CCM, kuwa ndio ilikuwa changamoto kubwa zaidi kwake ya kisiasa, baadhi ya wadadisi wa siasa za Zanzibar wanasema Oktoba itakuwa changamoto zaidi kwake. Dr Hussein Mwinyi, anakwenda kukabiliana na mwanasiasa mkongwe Maalim Seif Sharif Hammad, wa ACT-Wazalendo, ambaye amehudumu na baba yake rais mstaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi. Kutokana na kuwa na wafuasi wengi na mazingira ya chaguzi zote za Zanzibar toka kuanza mfumo wa vyama vingi Tanzania, kazi kubwa bado inamkabili Dr Mwinyi. Katika chaguzi zote za Zanzibar, Maalim Seif amekuwa akileta upinzani mkubwa kwa wagombea wote wa urais Zanzibar waliopita. Goodluck Nging’o ni mchambuzi wa siasa za Tanzania, na yeye pia analiona hilo.

“Ukiangalia Dr Mwinyi, mara nyingi amehudumu katika wizara za serekali ya muungano na kumfanya makazi yeke kuwa zaidi bara. Na ukimuangalia Maalim, yeye ni mwanasiasa mkongwe ambaye anaushawishi mkubwa visiwani hilo litaleta changamoto kwake. Lakini hii itategemea ataungana vipi na wenzake aliogombania nao kuomba urais ndani ya CCM, kama vile Shamsi Vuai Nahodha ambaye alihudumu kama waziri kiongozi wa Serekali ya Mapinduzi Zanzibar kwa miaka 10. Lakini zaidi ni historia yenyewe, mshindi wa uchaguzi Zanzibar hushinda kwa kura chahce zaidi ya mwenzake.” Alisema Goodluck Nging’o.

Lakini swali kubwa linabaki, Dr Hussein Mwinyi ni nani? Dr Mwinyi alizaliwa Desemba 23 mwaka 1966, visiwani Zanzibar, akiwa ni mmoja wa watoto 12 wa rais mstaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi.

Licha kuwepo na minong’ono ya kisiasa kwamba wadhifa wa baba yake ulimbeba, rais John Pombe Magufuli, ambaye ni mwenyekiti wa CCM, limuelezea Dr Mwinyi kuwa ni miongoni mwa watoto wa wakubwa waliojibeba wenyewe na kutojikweza.

Mwinyi kitaaluma ni daktari wa binadamu aliyesoma kiwango cha shahada ya uzamivu, ambaye masomo yake aliyapatia ndani na nje ya Tanzania, hasa Uturuki na Uingereza. Utoto wake amekulia na kusomea pia katika maeneo mbalimbali ikiwemo Misri, ambako baba yake alihudumu kama balozi wa Tanzania.

Nafasi za uongozi za baba yake zilizomfanya kuhama-hama na kuishi nje ya Zanzibar, zinafanya wapinzani wa Dr Mwinyi kuweka doa nafasi yake, kwa kudai si Mzanzibari kamili kwa kuwa makuzi na masomo yake kwa kiwango kikubwa yalikuwa nje ya Zanzibar. Kwa sasa ana mke na watoto kadhaa, na endapo atachaguliwa na wananchi wa Zanzibar, atakuwa rais Zanzibar kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG