Djibouti siku ya Jumatano ilitetea uamuzi wake wa kuwafukuza maafisa kutoka International Federation for Human Rights-Shirikisho la Kimataifa la Haki za Binadamu (FIDH) lenye makao yake mjini Paris, ikilishutumu kundi hilo la utetezi, kuwa na mapungufu ya kutoweka uwiano sawa katika kazi zake.
Alexis Deswaef, Makamu Rais wa FIDH alichukuliwa na maafisa katika hoteli aliyofikia siku ya Jumatatu baada ya kuwepo nchini humo kwa siku mbili na kupandishwa kwenye ndege kuelekea nchi jirani ya Ethiopia, kundi hilo limesema katika taarifa.
Siku moja kabla, mkurugenzi wa programu katika kundi hilo-hilo la FIDH, akiwa anatafuta ukweli wa tukio hilo wakati anatafuta Visa, alikataliwa kuingia katika uwanja wa ndege wa Djibouti na alipandishwa kwenye ndege kwenda Istanbul.
Polisi hawakutoa sababu ya kufukuzwa kwao. Lakini siku ya Jumatano, wizara ya mambo ya ndani ya Djibouti ilimshutumu Deswaef kwa kuwa wakili wa Daher Ahmed Farah, mwanachama wa upinzani ambaye amefungwa mara kadhaa na ambaye pia alilishtaki Jimbo la Djibouti mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.