Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Oktoba 07, 2022 Local time: 03:32

Uchafuzi wa mto Kongo wasababisha athari nyingi


Uchafuzi wa mto Kongo wasababisha athari nyingi

Ripoti kutoka shirika la MSF inasema watu wanapata ugonjwa wa kipindupindu kwa kutumia maji yasiyosafishwa

Uchafuzi wa maji ya mto Kongo umesababisha uhaba wa samaki jijini
Kinshasa na eneo la kusini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC.

Makampuni makubwa makubwa yamelaumiwa kumwaga takataka kwenye maji ya mto Kongo, huku serikali ikishindwa kuhakikisha hali bora ya ulinzi wa mazingira kwenye mto huo ambao una umuhimu mkubwa nchini humo kutokana na matumizi ya maji yake katika shughuli zote za maisha ya kila siku.

Mmoja wa wavuvi wa muda mrefu katika eneo hilo, Alfonso Mungulu alilalamika kwamba samaki wakubwa hivi sasa hawapatikani tena kwenye maji ya mto huo ulio kwenye bandari ndogo itwayo Kingabwa, kaskazini mwa jiji la Kinshasa, kutokana na kuchafuliwa kwa maji ya mto huo na wamekuwa wakipata samaki wadogo pekee aina ya dagaa.

“Nchi Kavu ya eneo hili ndio Quartier Limeté Indistruel ambako kumepatikana makampuni makubwa yanayotengeza pombe, kufua vyuma na shughuli nyingine kadhaa.”

Wakaazi wa Kingabwa wameshuhudia makampuni hayo yakimwaga takataka zao ndani ya maji ya mto Kongo. Madai ambayo yalitupiliwa mbali na baaadhi ya makampuni hayo. Japokuwa samaki mjini Kinshasa wana bei kubwa, lakini Samaki hao hawana ladha kutokana na uchafuzi huo wa maji ya mto Kongo.


Matumizi ya mifuko ya plastiki mjini humo na vilevile wakaazi ambao desturi yao ni kumwaga takataka za nyumbani ndani ya maji ya mto Kongo vimechangia pia katika uchafuzi wa maji ya mto Kongo .

Ripoti ya shirika la Medecins Sans Frontières inaeleza kwamba siasa mbovu ya uchafuzi wa maji ya mto Kongo kwenye eneo hili la kusini magharibi mwa nchi zimesababisha kuzuka kila mara kwa ugonjwa wa kipindupindu kutokana na watu wanaotumia maji yasiosafishwa ya mto Kongo.

Mbali na uvuvi wa samaki, maji ya mto Kongo yana umuhimu mkubwa kwa mamilioni ya wananchi wake ambao wanayatumia pia kama njia ya mawasiliano na kusafirishia bidhaa. Mto Kongo unaunganisha majimbo yote ya DRC, ispokuwa Kivu na Kassaï.

XS
SM
MD
LG