Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Julai 25, 2024 Local time: 16:16

CNDD-FDD yafurahishwa na idadi ya walojitokeza katika uchaguzi


Rais Pierre Nkurunziza, akisalimiana na wafuasi wa chama tawala nchini Burundi cha CNDD-FDD.
Rais Pierre Nkurunziza, akisalimiana na wafuasi wa chama tawala nchini Burundi cha CNDD-FDD.

Chama tawala nchini Burundi - CNDD-FDD - kinasema kimefurahishwa na jinsi watu walivyojitokeza katika uchaguzi wa bunge Jumatatu licha ya upinzani kususia na ukosoaji wa kimataifa kwamba mazingira ya upigaji kura hayakuwa huru, haki na ya wazi.

Msemaji wa chama Pascal Nyabenda alisema raia wa Burundi walikataa wito wa upinzani kususia kwa sababu wanapendelea demokrasia kuliko mapinduzi.

Upigaji kura ukiendelea Burundi
Upigaji kura ukiendelea Burundi

Alitupilia mbali ukosoaji wa dunia akisema serikali ilipanga uchaguzi kwa raia wa Burundi na waliitikia wito.“Kwa CNDD-FDD, tunaufurahia uchaguzi wa leo kwa sababu kulikuwa na idadi nzuri sana ya waliojitokeza na usalama ulikuwepo kila mahali nchi nzima,” alisema.

Bwana Nyabenda alikanusha madai kwamba upigaji kura uligubikwa na matokeo mabaya. Alisema ilitarajiwa kwamba baadhi ya vyama vya upinzani havitashiriki akiongeza kwamba raia wa Burundi walijitokeza kwa wingi kwa sababu wanataka demokrasia.

“Kile kinachowashangaza watu ni kwamba raia wa Burundi wanataka demokrasia hata kama viongozi wao wanasema wasipige kura. Bado, watu walikwenda kupiga kura ambapo inamaanisha kwamba hakuna uhusiano hivi sasa kati ya viongozi na baadhi ya wanachama wa baadhi ya vyama vya kisiasa,” alisema.

Umoja wa Afrika haukupeleka waangalizi kwa sababu ilisema hali ya uchaguzi haikuonekana kuwa huru, haki na uwazi.

Nkosazana Dlamini-Zuma
Nkosazana Dlamini-Zuma

Mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Afrika, Nkosazana Dlamini Zuma alielezea wasi wasi kuhusu kile alichokiita “hali mbaya sana ya kisiasa na usalama” nchini Burundi.

Wakati huo huo msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Mark Toner pia alielezea kutoridhika katika uchaguzi huo akisema ulikuwa umefanyika katika mazingira ya khofu na uchaguzi haukuwa huru na wa haki.

Lakini Nyabenda alisema kulikuwepo na waangalizi wengine kutoka Umoja wa Mataifa na Kenya. Pia alisema uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika Julai 15 utaendelea kama ulivyopangwa.

XS
SM
MD
LG