Wabunge wa Marekani Jumatano wamepuuza onyo kutoka ubalozi wa China kwamba wasikutane na rais wa Taiwan Tsai Ing-wen ambaye anatembelea California.
Kundi la wabunge 17 wa Marekani kutoka mirengo yote ya kisiasa wakiandamana na Spika wa bunge Kevin McCathy wamekutana na Tsai kwenye ukumbi na maktaba ya Ronald Reagan huko Simi Valley, California kwa kikao cha faragha. Saa chache kabla ya kikao hicho, chombo cha habari cha Punchbowl News kiliripoti kwamba baadhi ya wabunge hao walipokea barua pepe ikielekezea upinzani wa China wa kikao hicho pamoja na hatua inazoweza kuchukua. Msemaji wa mwakilishi Adam Curtis aliambia VOA kwamba China haiwezi kueleza wabunge wa Marekani ni nani wa kukutana naye kwenye ardhi ya Marekani. Kamati maalum ya bunge kwa ajili ya chama cha Kikomumisti cha China imekiambia VOA kwamba wabunge wengi waliokuwa wakielekea California kwa mkutano na rais Tsai waliripoti kupokea barua pepe.