Serikali ya Gambia inatetea kukamatwa kwa viongozi kadhaa wa upinzani na wafuasi wao.
Majibu haya yamekuja wakati katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa watu waliokamatwa. Marekani pia imelaani kile inachokiita majibu makali ya Serikali ya Gambia kufuatia maandamano ya karibuni ya Amani.
Vikosi vya usalama nchini Gambia siku ya Jumamosi vilimkamata Ousainou Darboe, kiongozi cha chama kikuu cha upinzani cha United Democratic Party (UDP), na baadhi ya wafuasi wake.
Pia kuna ripoti kwamba Solo Sandeng, katibu wa mipango kitaifa wa chama, aliteswa hadi kufa wakati akiwa chini ya ulinzi wa polisi.
Waziri wa habari wa Gambia, Sheriff Bojan amesema hajui lolote kuhusu mtu yeyote kuuwawa. Lakini alisema kiongozi wa upinzani Darboe na wafuasi wake walikiuka sheria ya Gambia kwa kufanya maandamano bila kibali kutoka kwa polisi.