Kundi la maafisa 11 likiongozwa na Baradine Berdei Targuio, kiongozi wa shirika la haki za binadamu la Chad, walipanga jaribio hilo, kulingana na taarifa ya serikali.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa idara za usalama ziliwakamata wahusika baada ya tarehe 8 Disemba.
Waziri wa habari akiwa pia msemaji wa serikali Aziz Mahamat Saleh amesema uchunguzi rasmi umeanzishwa kwa uvunjaji wa utaratibu wa katiba, kuunda kundi la uhalifu, kumiliki silaha kinyume cha sheria na kula njama.
Waziri Saleh ameongeza kuwa hakimu anayechunguza kesi hiyo amewafungulia mashtaka na ameamuru watiwe ndani.
Saleh amesema “Uchunguzi unafuata mkondo wake na serikali ina lengo la kufanya liwezekanalo kutoa mwanga kuhusu kesi hii na kubaini uwajibikaji.”
Mwezi Februari mwaka 2021, Targuio alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kwa mashtaka ya kudhoofisha utaratibu wa katiba kwa kuandika kwamba kiongozi wa wakati huo, Jenerali Idriss Deby Itno, alikuwa mgonjwa sana.
Facebook Forum