Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 09, 2024 Local time: 01:29

Callixte Nzabonimana ahukumiwa kifungo cha maisha jela


Fuvu za vichwa vya Wanyarwanda waliouawa mwaka wa 1994
Fuvu za vichwa vya Wanyarwanda waliouawa mwaka wa 1994

Nzabonimana alichochea hadharani mauaji dhidi ya Watutsi

Mahakama ya uhalifu wa kivita kwa ajili ya Rwanda imemhukumu kifungo cha maisha jela afisa wa zamani wa Rwanda Callixte Nzabonimana kwa mauaji ya halaiki. Mahakama hiyo ya kimataifa kwa ajli ya Rwanda ilisema waziri huyo wa zamani alichochea mauaji ya watu kati ya 15 hadi 60 wa kabila la Tutsi mwezi Aprili mwaka wa 1994 katika eneo la Nyabikenke. Ilisema pia kuwa alichochea watu mara tatu hadharani mwezi huo kuwauwa Watutsi na akaingia kwenye makubaliano ya kuwauawa watu wa kabila hilo na serikali ya muda ya Rwanda wakati huo. Nzabonimana alikuwa waziri wa maswala ya vijana wa Rwanda katika serikali ya muda iliyoundwa mwaka wa 1994. Alikamatwa mwezi Februari nchini Tanzania na kukabidhiwa mahakama ya kimataifa ya uhalifu kwa ajili ya Rwanda yenye makao yake mjini Arusha, Tanzania. Wanamgambo wa Kihutu inakisiwa waliuawa watu laki 8 wa kabila la Tutsi na Wahutu wenye msimamo wa kadri wakati wa mauaji ya halaiki mwaka huo wa 1994. Mahakama hiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ilibuniwa kwa ajili ya kusikiliza kesi dhidi ya wahusika wakuu wa mauaji ya halaiki ya Rwanda.

XS
SM
MD
LG