Aliyekuwa mkuu wa upelelezi nchini Burundi, Luteni Jenerali Adolphe Nshimirimana ameuawa Jumapili asubuhi katika mji mkuu Bujumbura. Bwana Nshimirimana alishambuliwa akiwa ndani ya gari lake kwenye makutano ya barabara ya kaskazini na katikati mwa mji mkuu.
Kwa mujibu wa habari kutoka Bujumbura dereva na mlinzi wake ni miongoni mwa waliouawa. Walioshuhudia wamesema waliofanya shambulizi hilo walikuwa wamevalia sare za jeshi.
Mkuu wa idara ya mawasiliano katika Ikulu, Willy Nyamitwe amethibitisha kifo cha Nshimirimana lakini hakutoa maelezo zaidi kuhusu tukio hilo. Mkuu wa huyo wa zamani wa upelelezi pia aliwahi kuwa naibu mkuu wa majeshi ya Burundi mwaka 2005 baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kumalizika nchini humo kufuatia mkataba wa amani wa Arusha na baadaye kuteuliwa kushika wadhifa wa mkuu wa idara ya ujasusi. Na hivi sasa alikuwa akishikilia wadhifa wa mshauri katika ofisi ya rais.