Majeshi ya Burkina Faso yameingia katika mji mkuu, Ougadougou, kufanya mazungumzo kuhusu kujisalimisha kwa wakuu wa mapinduzi ya hivi majuzi, wakati balozi wa Ufaransa anasema rais wa muda Michel Kafando ameachiliwa.
Taarifa ya jeshi imesema wanajeshi wameingia mjini humo katika jaribio la kumaliza mapinduzi wa serikali bila umwagaji damu.
Jumatatu, kiongozi wa mapinduzi Jenerali Gilbert Diendere alisema katika taarifa kuwa atawachia madaraka kama kiongozi wa nchi mwishoni mwa mazungumzo yanayosimamiwa na Jumuiya ya Uchumi ya ECOWAS.
ECOWAS inafanya mkutano wa dharura nchini Nigeria kujadili hali ya Burkina Faso.
Jenerali Diendere, ambaye ni kiongozi wa kikosi cha ulinzi wa rais, alichukua madaraka na kumshikilia Rais Kafando Jumatano iliyopita. Ameomba radhi kwa taifa na anasema anapanga kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia.