Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amesema kuwa kikosi cha pamoja cha kupambana na kundi la Boko Haram kitakuwa kimeanza kazi yake kufikia mwisho wa mwezi huu.
Kwenye mahojiano Jumanne na Peter Clottey wa VOA, Bw Buhari amesema Nigeria itakua mstari wa mbele na kwamba vikosi kutoka Chad, Niger, Nigeria na Benin vitawekwa kwenye operesheni dhidi ya wanamgambo hao.
Bw Buhari yuko katikati ya ziara yake ya siku nne mjini Washington. Amekutana na Waziri wa Mambo ya nNe wa Marekani John Kerry Jumanne kabla ya kufanya vikao na wajumbe wa Congress na wa Nigeria wanoishi Marekani.
Jumatatu, kiongozi huyo wa Nigeria alikutana na rais Barack Obama huko White House. Bw Obama amesifu uchaguzi wa hivi karibuni nchini Nigeria ambao ulitoa nafasi ya mpito ya uongozi wa kidemokrasia tangu mwisho wa utawala wa kijeshi 1999.