Polisi wanamtaka Nathan L’okori kutoa ushahidi kwamba spika Jacob Oulanya alipewa sumu.
Msemaji wa Polisi Fred Enanga, ameambia waandishi wa habari Jumatatu kwamba L’Okori na viongozi wengine kadhaa wametakiwa kujiasilisha kwa polisi kwa mahojiano.
Viongozi hao ni pamoja na aliyekuwa mgombea wa urais Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, aliyekuwa waziri wa utalii ambaye pia ni naibu wa chama kinachotawala cha National resistance movement (NRM) Godfrey Kiwaanda, waziri wa habari na teknolojia Chris Baryomunsi, mbunge Gilbert Oulanyah, na viongozi wengine wa jamii ya Acholi.
Kulingana na polisi, hakuna ushahidi kwamba Jacob Oulanya aliuawa kwa kupewa sumu.
Ripoti ya madaktari
Kulingana na ripoti rasmi ya madaktari wa hospitali ya chuo kikuu cha Washington, nchini Marekani, Jacob Oulanya alifariki baada ya viongo kadhaa mwilini mwake kukosa kufanya kazi.
Lakini wakati wa mazishi babake Oulanya, L’Okori alisisitiza kwamba aliambiwa na mtoto wake kwamba alipewa sumu.
“Siombolezi kwa uchungu bila sababu. Nataka kueleza bayana kwamba Jacob alipewa sumu. Aliniambia mwenyewe. Alifanyiwa upasuaji. Sumu hiyo iliathiri afya yake vibaya sana. Wakati alipelekwa nje ya nchi kwa matibabu, hakuwa katika hali ambayo angepona. Alikuwa amedhoofika sana.” L’Okori alisema akiongezea kwamba “nyinyi waombolezaji, tafadhali pokeeni habari hizi kwa nia njema. Mwanangu amekufa. Ameenda. Hatutamuona tena.”
Kiongozi wa chama kinachotawala NRM, aendeleza madai ya sumu
Siku iliyofuatia (Jumamosi April 9, 2022), aliyekuwa waziri wa utalii, ambaye pia ni naibu wa mwenyekiti wa chama kinachotawala cha NRM Godfrey Kiwanda, akiwa katika kipindi cha radio maarufu nchini Uganda – Capital Gang, kwenye Capital FM, alisema kwamba aliambiwa na Jabob Oulanya kwamba alikuwa amepewa sumu.
“Alipochaguliwa, nilimpigia simu. Alinialika nyumbani kwake na tulikuwa na mazungumzo. Nilimpata kitandani na alikuwa anaugua sana. Aliniambia, Godfrey, nilipewa sumu, lakini usimwambie mtu yeyote.”
Kiwanda alisema kwamba alimuuliza Oulanya kuhusu anayeamini au kudhani alimpa sumu na kajibubu, “Sina habari.”
Aliongezea kwamba hakunyamazia habari hizo. Alimwambia waziri wa habari na teknolojia Chris Baryomunsi ili uchunguzi ufanyike.
Mbona Bobi Wine ameitwa na polisi?
Bobi Wine, alitoa wito kwa serikali kufanya uchunguzi wa haraka kuhusiana na madai kwamba Oulanya alipewa sumu.
“Nilineda kumtembelea baba ya Oulanya kumpa pole zangu. Ujumbe wa baba ya Oulanya kuhusu mtoto wake kupewa sumu umesikika vizuri sana. Kwa hivyo, tunataka serikali kufanya uchunguzi wa haraka sana,” Bobi waine alisema hayo baada ya kutembelea baba yake nyumbani kwake.
Polisi wasema waliotoa mdai ya Oulanyah kupewa sumu lazima watoe maelezo zaidi
Kulingana na msemaji wa polisi Fred Enanga, hakuna mahali popote katika ripoti ya madaktari, kuonyesha kwamba Oulanya alipewa sumu na kwamba waliotoa madai hayo lazima watoe habari zaidi.
“Madai yoyote yanayotolewa kuhusu kilichosababisha kifo cha Oulanya kando na ripoti ya madaktari, ni uvumi ambao ni hatari sana” akiongezea kwamba “kwa hivyo tumewaita watu waliotoa madai hayo ili watueleze kile ambacho hatujui.”
Hatua ya polisi inatokana na amri ya rais Yoweri Museveni kutaka polisi kuwakamata watu wanaodai kwamba aliyekuwa spika wa bunge la taifa Jacob Oulanya alipewa sumu.
Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC