Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amekutana na Mwanamfalme Faisal bin Farhan, waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia na mawaziri wa mambo ya nje kutoka Baraza la Ushirikiano wa Ghuba kama sehemu ya ziara yake nchini Saudi Arabia.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema wanadiplomasia wa Marekani na Saudi Arabia walijadili masuala kadhaa kati ya nchi hizo mbili pamoja na masuala ya kikanda na kimataifa.
Waziri Blinken na waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia wameazimia kuendelea kufanya kazi pamoja kukabiliana na ugaidi, kuunga mkono juhudi za kuleta amani ya kudumu nchini Yemen, na kukuza utulivu, usalama, kupunguza mivutano na kukuza ushirikiano katika kanda hiyo, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Matthew Miller amesema.
Pande hizo mbili zimeahidi kuendeleza ushirikiano wao wa dhati ili kumaliza mapigano nchini Sudan. Marekani na Saudi Arabia zimekuwa zikiongoza mazungumzo mjini Jeddah kama wapatanishi kwenye mzozo wa Sudan lakini zimeshindwa kupata makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano kati ya makundi yanayohasimiana.
Forum