Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Juni 20, 2024 Local time: 14:44

Bensouda aapishwa kama mwendesha mashtaka mkuu wa ICC


Bensouda ni mwanamke wa kwanza wa Afrika kupewa cheo hicho

Wakili wa Gambia Fatou Bensouda ameapishwa kama mwendesha mashtaka mkuu mpya wa mahakama ya kimataifa inayosikiliza kesi za uhalifu –ICC. Bensouda mwenye umri wa miaka 51 alikula kiapo katika sherehe zilizofanyika Ijumaa mjini The Hague. Bensouda ni mwanamke wa kwanza Mwafrika kupewa jukumu la mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama hiyo ya ICC, ambayo wengi wameshtumu wakisema inafuatilia kesi za uhalifu kutoka nchi za Afrika pekee. Bensouda, katika mahojiano wiki hii alipinga shtuma hizo akisema kuwa yeye binafsi anawahudumia waathiriwa wa Afrika. Amechukua nafasi ya Louis Moreno-Ocampo wa Argentina aliyestaafu kama mwendesha mashtaka mkuu Ijumaa baada ya kuhudumu katika cheo hicho kwa miaka 9. Kabla ya kujiunga na mahakama hiyo ya kimataifa, Bensouda alikuwa mshauri mkuu wa kisheria katika mahakama ya kimataifa kwa ajili ya Rwanda. Hapo awali alikuwa mkuu wa sheria wa Gambia. Mahakama ya kimataifa ICC ilianzishwa mwaka wa 2002 kusikiliza kesi za uhalifu wa kimataifa na uhalifu dhidi ya binadamu pamoja na mauaji ya halaiki. Kwa sasa mahakama hiyo inafuatilia kesi 15 kutoka nchi saba za Afrika zinazohusu maafisa wa ngazi za juu.

XS
SM
MD
LG