Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Agosti 17, 2022 Local time: 13:34

Benin na Chad wapiga kura, wapinzani wadai kutengwa


Rais aliyeko mdarakani wa Benin Patrice Talon akipiga kura yake huko katika kituo cha Zongo Ehuzu katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo. April 11, 2021. Rais Patrice Talon anagombea muhula wa pili (Photo by PIUS UTOMI EKPEI / AFP)

Kazi ya kuhesabu kura inafanyika Chad na Benin ambako wapiga kura katika nchi hizo mbili za magharibi mwa Afrika walipiga kura Jumapili kwenye uchaguzi wa urais ambapo wanasiasa wa upinzani wanadai walizuiwa kushiriki.

Idriss Deby Itno wa Chad, akichanganya mbinu kali na ujuzi wa kisiasa, amewaweka kando wapinzani wake wenye nguvu, akiwa njiani kuelekea kwenye muhula wa sita kama rais baada ya miaka 30 katika uongozi wa taifa lake.

Nchini Benin Rais Patrice Talon alionekana atashinda uchaguzi wa pili Jumapili baada ya kura ya mvutano mkali, huku wakosoaji wakimtuhumu kuiba uchaguzi huo kwa kuwatenga viongozi wa upinzani.

Rais Patrice Talon wa Benin, tajiri wa pamba aliyechaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2016, alikabiliana na wapinzani wawili wasiojulikana wakati viongozi wengine wakuu wa upinzani wa nchi hiyo walisusia uchaguzi huo.

Benin wakati mmoja ilisifiwa kama nchi yenye demokrasia yenye nguvu katika eneo lenye changamoto, lakini idadi kubwa ya wapinzani sasa wako uhamishoni au wamekataliwa na tume ya uchaguzi au wamelengwa kwenye uchunguzi na mahakama maalum.

Mvutano uliongezeka kabla ya kura, na maandamano yalizuka katika miji kadhaa katika ngome za upinzani ingawa upigaji kura uliendelea kwa amani Jumapili.

Wafuasi wa Talon wamekataa shutuma za kuwa uchaguzi utaibiwa , wakisema hali imewekwa sawa kwa kura ya haki.

Rais wa tume ya uchaguzi Emmanuel Tiando aliambia shirika la habari la AFP Jumamosi kuwa licha ya ucheleweshaji wa kupeleka vifaa vya uchaguzi kaskazini, hakuna chochote kinachozuia uchaguzi huo kufanyika.

Zaidi ya watu milioni 4.9 wanastahiki kupiga kura katika vituo zaidi ya 15,500. Matokeo ya mwisho hayatarajiwa hadi Jumatatu au Jumanne. Christian Tchogninou, mwakilishi wa chama cha rais Talon anasema kila kitu kilienda sawa Jumapili.

Huko Chad, rais Idriss Deby Itno, mtawala kwa miaka 30 iliyopita, anajiandaa kushinda muhula wa sita. Mshirika huyo muhimu katika kampeni ya Magharibi ya kupambana na kundi la jihadi huko Sahel, Deby, mwenye umri wa miaka 68, ndiye anayeongoza katika kinyang'anyiro cha wagombea sita bila wapinzani wakuu na baada ya kampeni ambayo maandamano yalipigwa marufuku au kutawanywa.

Akizungumza na waandishi wa habari alipopiga kura yake katika kituo kikuu cha kupigia kura katika mji mkuu N'Djamena, Deby alitoa mwito kwa wanaume na wanawake wote wa Chad popote walipo kujitokeza kwa wingi na kupiga kura, huku akipuuzia wito wa vyama vya upinzani kususia uchaguzi.

Katika nchi hizo mbili wapiga kura wamegawanyika kwa karibu masuala sawa.Chad imepambana na umaskini na ukosefu wa utulivu tangu kupata uhuru wake kutoka kwa Ufaransa mwaka 1960.

Mwanajeshi mwasi wa zamani ambaye alitwaa madaraka katika mapinduzi mwaka 1990, Deby alifanikiwa mara mbili, kwa msaada wa Ufaransa, alizuia majaribio ya kumwondoa mamlakani.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG