Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Oktoba 01, 2023 Local time: 13:08

Bashir awasili Khartoum akikwepa kukamatwa Afrika Kusini


Rais wa Sudan, Omar al-Bashir, wa pili kulia akiwa na viongozi wenzake katika mkutano wa AU huko Johannesburg, June 14 2015.

Rais wa Sudan Omar al-Bashir alisafiri kwa ndege kutoka Afrika kusini jumatatu akikaidi amri ya mahakama ya Pretoria aendelee kukaa nchini humo hadi uamuzi utolewe kama akamatwe kuhusiana na mashtaka ya uhalifu wa vita na mauaji ya halaiki.

Bwana Bashir alikuwa Afrika kusini kuhudhuria mkutano wa umoja wa Afrika, lakini mahakama ya kimataifa ya uhalifu-ICC ilitaka akamatwe wakati akiwa huko. ICC imemfungulia mashtaka ya mauaji ya halaiki, uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya binadamu kwa kutuma jeshi na kuwaunga mkono wanamgambo wa kiarabu kuzima uasi wenye silaha huko Darfur wakati wa mgogoro wa mwaka 2003 lakini bwana Bashir kwa muda mrefu anakaidi amri ya mahakama.

Rais wa Sudan, Omar al-Bashir
Rais wa Sudan, Omar al-Bashir

Shirika rasmi la habari la Sudan lilisema bwana Bashir atafanya mkutano na waandishi wa habari kwenye uwanja wa ndege wa Khartoum wakati akiwasili jumatatu usiku kwa saa za Sudan.

Kabla bwana Bashir kuondoka Afrika kusini, wote Umoja wa mataifa na Marekani walitaka akamatwe.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon alisema “mamlaka ya ICC lazima yaheshimiwe na uamuzi wake utekelezwe”.

Mapema jumatatu waziri wa habari wa Sudan alisema bwana Bashir atarudi nyumbani bila shaka mwishoni mwa mkutano licha ya amri ya jaji mmoja wa Afrika kusini akitoa wito kwa maafisa wamzuie kuondoka nchini humo.

Waziri wa habari wa Sudan, Ahmed Bilal Osman aliiambia Sauti ya Amerika-VOA kwamba rais “sio mhalifu” na alihudhuria mkutano baada ya kupata uhakikisho kutoka kwa Rais wa Afrika kusini, Jacob Zuma kwamba hatokamatwa. “Tuna uhusiano mzuri na serikali ya Afrika kusini” alisema Osman. “Tunajua kwamba hawatamkamata rais na hakuna kitu chochote kitakachotokea”.

Osman pia aliikosoa ICC ambayo bado ina kesi hai inayoihusisha Sudan, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC, Jamhuri ya Afrika ya kati, Kenya, Libya na Ivory Coast.

“ICC ni mahakama inayofanya kazi moja kwa moja kuelekeza adhabu kwa viongozi wa Afrika. Uhalifu mwingi hivi sasa umefanyika duniani kote na nchi hizi zimepata kinga”, alisema Osman hususan akiilenga Israel na Marekani.

Wakati huo huo msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, John Kirby alisema kwamba wakati Marekani sio sehemu ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu inaunga mkono vikali juhudi za kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wale waliohusika kwa mauaji ya halaiki na uhalifu wa vita.“Katika janga la ukatili huko Darfur tunatoa wito kwa serikali ya Afrika kusini kuunga mkono juhudi za mahakama ya kimataifa ya uhalifu kuwapatia sheria waathirika wa uhalifu huu mbaya, Kirby alisema katika taarifa yake.

Umoja wa Mataifa unasema mapigano katika eneo la Darfur yameuwa watu 300,000 na kusababisha wakimbizi zaidi ya milioni mbili. Wengi wa waathirika walikuwa raia.

Rais wa ICC, Sidiki Kaba alisema Afrika kusini ambayo muda wote inachangia kuboreshwa kwa mahakama hiyo haitakiwi kuzuia juhudi za kuhakikisha inatekeleza hati za kukamatwa.

Licha ya wito wa kukamatwa kwake bwana Bashir alijumuika katika picha ya pamoja na viongozi wengine wa Afrika kwenye mkutano huo mjini Johannesburg hapo jumapili.

XS
SM
MD
LG