Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Machi 28, 2024 Local time: 12:33

Ban Ki-moon alaani ubakaji Kivu Kaskazini


Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon

Katibu mkuu wa Umoja Mataifa Ban Ki-moon, alisema Jumatano amekasirishwa sana na ubakaji na mashambulizi ya zaidi ya wanawake 150 huko Kivu Kaskazini, DRC

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon anamtuma afisa wa cheo cha juu wa Umoja wa Mataifa kwenda kuchungza mashambulizi hayo na ubakaji wa zaidi ya wanawake 150 Kivu Kaskazini huko DRC. Bwana Ban anasema ubakaji huo wa wanavijiji ulifanywa na wapiganaji wenye silaha wa makundi mawili ya waasi. Alieleza mashambulizi hayo kuwa mfano mwengine mbaya wa kiwango cha ghasia za ngono na ukosefu wa usalama unaokumba Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Martin Nesirky akisoma taarifa ya Bw. Ban alisema,
“Katibu mkuu anarudia wito wake wakutaka makundi yote yenye silaha huko DRC, kuweka chini silaha zao, na kuungana na utaratibu wa amani. Katibu mkuu pia anatoa wito kwa serikali ya congo kuchunguza tukio hilo na kuwafikisha wahusika wa uhalifu huo mbele ya sheria, na kuanzisha tena juhudi za kumaliza ukosefu wa usalama mashariki mwa nchi hiyo.”

Wakati huo huo Bw Ban anamtuma naibu Katibu Mkuu wa masuala ya kulinda amani Atul Khare, kwenda DRC kuchunguza mashambulizi hayo. Naye Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya ghasia za ngono Margot Wallstrom, amepewa jukumu la kusimamia namna Umoja wa Mataifa utakabiliana na tatizo hilo.

Anasema mashambulizi ya Kivu Kaskazini yanathibitisha uchunguzi wake wakati wa ziara yake ya hivi karibuni huko DRC, juu ya kuenea kwa mpangilio wa ubakaji na ukiukaji mwengine wa haki za binadamu nchini humo.

Kulingana na ripoti za habari, mashambulizi ya waasi yalifanyika baina ya tarehe 30 Julai na Agosti 3. Umoja Mataifa unasema kuwa kuna kambi ndogo ya kikosi cha amani takriban kilomita 30 kutoka kijiji hicho. Lakini kulingana na msemaji Martin Nersirky, waasi waliwafungia njia wanavijiji, na hawakuweza kwenda kuripoti mashambulizi kwa watu wa nje.

Kulingana na Nersirky, walinda amani walipata habari za ubakaji huo kutoka kwa mfanyakazi wa huduma za afya hapo Agosti 12, wiki mbili baada ya tukio hilo kutendeka.

XS
SM
MD
LG