Baadhi ya shule nchini Marekani iliongeza muda wa mapumziko yao ya likizo wiki hii, au ikarejea kwenye mafunzo kwa njia ya mtandao, kwa sababu ya ongezeko la maambukizi ya COVID-19, huku zingine zikisonga mbele na masomo ya ana kwa ana.
Hayo yanafanyika huku kukiwa na hisia kuwa Wamarekani watalazimika kujifunza kuishi maisha yao huku Covid 19 ikiendelea kuwepo. Walipokumbana na maombi kutoka kwa walimu wanaoogopa kuambukizwa na wazazi wanaotaka watoto wao darasani, maafisa wa idara za elimu katika miji kama vile New York, Milwaukee, Chicago, Detroit na kwingineko walijikuta katika hali ngumu katikati ya mwaka wa masomo, kwa sababu ya maambukizi kuongezeka.
Jiji la New York, ambalo ndilo lenye mfumo mkubwa zaidi wa shule nchini, lilifungua tena madarasa kwa takriban wanafunzi milioni 1, wakiwa na akiba ya vifaa vya kufanyia vipimo ya COVID-19, na linapanga kuongeza mara mbili idadi ya vipimo vya papo hapo, vinavyofanywa shuleni.