Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat alisema Ijumaa kwamba chombo hicho kitakutana kuzungumzia kama kiondoe sitisho la muda kwa Mali, Burkina Faso na Guinea ambazo zina utawala wa kijeshi.
Mataifa yote matatu yamesimamishwa kwa muda uanachama wao katika Umoja wa Afrika pamoja na Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) baada ya mapinduzi ya kijeshi tangu mwaka 2020 na hivyo hayawezi kushiriki katika mkutano wa kilele wa mwishoni mwa wiki hii unaofanyika katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.
"Suala hili bado halijajadiliwa, kutakuwa na mkutano wa Baraza la Amani na Usalama ambao utaangalia maombi haya, kwa hivyo bado hakuna uamuzi kwa maana hii," Faki aliliambia shirika la habari la AFP bila kutaja muda.
Wanadiplomasia wa nchi za Afrika Magharibi walianza kuzipigia debe nchi zao kurejeshwa katika umoja huo wenye nchi wanachama 55 na walikutana alhamisi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Comoro, Dhoihir Dhoulkamal ambaye nchi yake itashikilia urais wa kupokezana wa AU.
Facebook Forum