Umoja wa Afrika na jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika magharibi-ECOWAS wanatuma timu ya pamoja ili kujaribu kusitisha ghasia nchini Senegal kabla ya uchaguzi wa rais utakaofanyika Jumapili.
Rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo anaongoza timu hiyo. Mkurugenzi wa mawasiliano wa ECOWAS, Sonny Ugoh aliiambia Sauti ya Amerika kwamba licha ya mapambano yanayosababisha vifo kati ya waandamanaji na majeshi ya usalama, hali hiyo inaweza kutatuliwa kupitia mazungumzo.
Maafisa wa usalama walisema mtu mmoja aliuwawa Jumapili katika mji wa Kaolack wakati waandamanaji walipopambana na polisi juu ya hatua ya rais Abdoulaye Wade ya kuwania muhula wa tatu madarakani.
Upinzani unaoongozwa na kundi la M23, unasema Bwana Wade hastahili kugombea tena kutokana na kithibiti cha katiba kinachoelezea mihula miwili ya kuwepo madarakani. Lakini mwezi uliopita mahakama kuu nchini Senegal ilisema kidhibiti hicho hakimkatazi Wade kwa kuwa alikuwa tayari madarakani wakati uamuzi ulipopitishwa.
Watu wasiopungua sita wamekufa katika mapambano ya mitaani tangu ghasia zilipoanza baada ya hatua hiyo ya mahakama.
Msemaji wa kampeni za uchaguzi za Bwana Wade aliambia Sauti ya Amerika kuwa anaimani Rais atashinda uchaguzi wa Jumapili. “Sina shaka lolote kwamba Rais Wade atashinda kwenye mzunguko wa kwanza. Hatutakuwa na mzunguko wa pili kwa sababu anapendwa na watu wa Senegal. Anafanya kazi sana, na anafanya kazi vizuri mno. Kila mahali unapokuwepo, unaona kitu kinachomtambua Rais Wade.”
Marekani na Ufaransa wanamsihi bwana wade, ambaye ana umri wa miaka 85 kukabidhi madaraka ili kutoa mwanya kwa kizazi cha vijana.
Rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo anaongoza timu ya AU na ECOWAS inayojaribu kusitisha ghasia zinazoendelea nchini Senegal