Maafisa wa usalama na mashahidi wanasema wanajeshi wa serikali ya Somalia wamekomboa tena kijiji cha Goofgaduud kusini mwa Somalia baada ya wanamgambo wa Alshabab kuchukua kwa muda mfupi udhibiti wa kijiji hicho Jumapili.
Naibu mkuu wa polisi Mohamed Isaq Ara’as ameiambia sauti ya Amerika kwamba wanamgambo walishambulia kambi ya kijeshi na hapo wanajeshi wakaondoka ili kupanga mkakati na kuwashambulia tena wanamgambo hao na kuchukua udhibiti wa kijiji hicho muhimu.
Alisema wanajeshi wanne wa serikali na wanamgambo wanane waliuwawa wakati wa mapigano na wanamgambo wengine 10 walijeruhiwa.
Goofgaduud iko kiasi cha kilometa 250 kaskazini magharibi mwa mji mkuu Mogadishu katika eneo ambalo wanamgambo na wanajeshi wa serikali walipambana mara kadhaa katika siku za nyuma.