Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Aprili 18, 2024 Local time: 06:19

Aliyekuwa rais wa Burkina Faso ahukumiwa maisha gerezani kwa kumuua Sankara


Aliyekuwa rais wa Burkina Faso Blaise Compaore, anayeishi uhamishoni Ivory Coast. Picha: AFP
Aliyekuwa rais wa Burkina Faso Blaise Compaore, anayeishi uhamishoni Ivory Coast. Picha: AFP

Mariam Sankara, mjane wa rais wa zamani wa Burkina Faso, Thomas Sankara, anasema hatimaye amepata ahueni kwa sababu sasa anajua ukweli, baada ya mahakama ya kijeshi kutoa hukumu ya maisha kwa waliohusika na mauaji ya mumewe mwaka 1987, ikijumuisha rais wa zamani Blaise Compaore.

Akiongea na wanahabari nje ya mahakama baada ya uamuzi kutangazwa, Prospere Farama, wakili wa upande wa mashtaka amesema kwamba hatimaye haki imepatikana. Kwa sababu imechukuwa miaka 34 ya manyanyaso dhidi ya watu. Amesema kwamba hatupaswi kusahau, kwamba imechukuwa miaka 34 kwa raia wa Burkina Faso kupambana na udhalimu, na kwa hukumu hiyo umekuwa ni ushindi mkubwa kwa watu.

Mahakama ya kijeshi ya Burkina Faso, Jumatano imetoa hukumu ya kifungo cha maisha kwa rais wa zamani Blaise Compaore kwa kuhusika na mauaji ya mwaka 1987 ya aliyekuwa rais mwanamapinduzi Thomas Sankara.

Makofi yalipigwa katika mahakama wakati hukumu iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu iliposomwa, na kuifunga kesi iliyokuwa ikipuuzwa na serekali dhalimu kwa kipindi cha miaka 34.

Mwanajeshi aliyeongoza mapinduzi naye ahukumiwa

Mahakama pia imetoa hukumu ya kifungo cha maisha kwa Hyacinthe Kafando, afisa anaye shukiwa kuongoza kikundi cha mauaji, na Jenerali Gilbert Diendere kamanda wa jeshi wa wakati wa mauaji ambayo yaliendana na mapinduzi yaliyomuweka madarakani rais Compaore.

Rais huyo wa zamani Compaore, anaishi uhamishoni nchini Ivory Coast, baada ya kuondolewa na maandamano makubwa ya umma mwaka 2014, na Kafando ambaye amekimbia toka mwaka 2016 walihukumiwa bila ya kuwepo mahakamani.

Kesi hiyo iliyokua inasikilizwa kwa muda wa miezi sita ilikuwa ikifuatiliwa kwa karibu katika taifa hilo la Sahel, ambalo kifo cha Sankara kimebaki kuwa dosari baya katika historia yake.

Mauaji ya Sankara

Kiongozi aliyekuwa na msimamo wa kimapinduzi na mtazamo wa Marxist-Leninist ambaye alikuwa akishutumu ukoloni mamboleo na unafiki, Sankara aliuwawa kwa kufyatuliwa risasi Oktoba 15, 1987, baada ya kipindi cha muda mfupi chini ya miaka minne toka alipoingia madarakani akiwa kapteni wa jeshi mwenye umri wa miaka 33.

Yeye na wenzake 12 waliuwawa na kikosi cha mauaji wakati wa mkutano baraza la mapinduzi la kitaifa.

Kujadiliwa kwa kifo cha kiongozi huyo aliyekuwa na mrengo wa kushoto lilikuwa ni jambo lisilo kubaliwa katika kipindi cha miaka 27 ya utawala wa Compaore ambaye alikuwa mwanaharakati mwenzake na Sankara.

Mahakama katika mji mkuu wa Ouagadougou umemkuta Compaore, Kafando na Diendere na hatia ya kudhuru usalama wa nchi.

Compaore na Diendere walikutwa na hatia ya kupanga mauaji, na Kafando ya mauaji.

Hukumu ndefu kuliko maombo ya waendesha mashtaka

Hukumu yao ni ndefu zaidi kuliko maombi ya waendesha mashitaka wa jeshi. Walipendekeza miaka 30 kwa Compaore na Kafando, na miaka 20 Diendere, ambaye tayari anatumikia kifungo cha miaka 20 kwa kujaribu kufanya mapinduzi mwaka 2015.

Wengine wanane walio shutumiwa walipewa hukumu yenye kipindi cha kuanzia miaka mitatu mpaka 20 gerezani huku washtakiwa watatu wakifutiwa mashitaka.

XS
SM
MD
LG