Katika hotuba yake kwa wajumbe wanaohudhuria mkutano wa viongozi wa wajasiriamali hapa Washington Rais Barack Obama alitangaza mipango mipya yenye lengo la kuwaleta pamoja wajasiriamali, ili waweze kubadilishana ujuzi kati yao na kufahamiana zaidi.
“Marekani inazindua miradi mipya kadhaa. Tutawaleta wajasiriamali wa biashara na masuala ya kijamii kutoka mataifa ya kislamu hadi Marekani na tutawapeleka wenzao wa kimarekani kusoma katika mataifa yenu”.
Rais Obama, alitangaza pia mpango mpya wa kuwasaidia wanawake katika fani za teknolojia ambao watakua na nafasi ya kuja Marekani kwa ajili ya kupata uzoefu na maendeleo ya kufanya kazi kwa ustadi zaidi.
“Na kwa vile uvumbuzi ni kiini cha ujasiriamali, tutabuni mradi mpya wakubadilishana walimu wa sayansi. Tunaanzisha ushirikiano mpya ambapo viongozi wa teknolojia ya juu kutoka makampuni ya Silicon Valley wataweza kueleza ujuzi wao katika teknolojia, biashara na uongozi pamoja na washirika wao huko Mashariki ya Kati, Uturuki na Asia Kusini.”
Kiongozi wa Marekani, amesema mfuko wa teknolijia ya kimataifa alioutangaza mwaka jana huko Cairo una uwezekano wa kukusanya dola bilioni 2 kutoka kwa wawekezaji binafsi kutoka sekta kama vile mawasiliano ya simu, huduma za afya, elimu na miundo mbinu. Rais obama alitangaza kwamba mkutano wa pili juu ya ujasiriamali utafanyika mwakani huko uturuki.