Maafisa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC, wanaendelea kuchunguza kwa makini mlipuko wa Volkano katika mlima Nyamulagira.
Jana Jumapili volcano hiyo ilirusha majivu ya moto karibu na mbuga ya wanyama ya Virunga iliyo karibu na kutishia maisha ya wanyama kama vile Sokwe Mtu na wanyama pori wengine wanaoishi kwenye mbuga hiyo.
Mlipuko huo bado haujaathiri wakazi wanaoishi karibu na eneo, lakini maafisa wana khofu kuwa majivu yanayotokana na volcano hiyo huenda yakadhuru maji yanayotumiwa na jamii na wanyama wanaoishi karibu.
Mamlaka za wanyama pori huko DRC, zinasema kuwa mlipuko wa volcano kutoka mlima Nyamulagira, huenda ukawadhuru Sokwe Mtu wapatao 40, ambao tayari maisha yao yamo hatarini. Volkano hiyo imo kilomita 22 kutoka mji mkuu wa Goma, ulioko katika jimbo la Kivu kaskazini nchini DRC.