Mjitoa mhanga alilipua gari lililojaa milipuko kwenye uwanja wakati wa mchuano wa mpira wa wavu kaskazini mashariki mwa Pakistan, na kuwaua watu 88. Maafisa wa usalama wanasema, watu wengine kadhaa walijeruhiwa wakiwemo watoto.
Shambulio hilo lililotokea Ijumaa ni la tatu kuu, lililofanywa na wanaharakati nchini humo mnamo wiki hii na kusababisha zaidi ya vifo vya watu 120. Shambulio hilo kubwa lilitokea katika kijiji cha mbali, karibu na mji wa Lakki Marwat, huko kaskazini mashariki ya Pakistan.
Akizungumza na Sauti ya Amerika kwa njia ya simu, mkuu wa polisi wa mkoa Malik Naveed, alieleza kwamba gari lililokua limejazwa kiasi cha kilogram 100 hadi 300 za milipuko liliendeshwa moja kwa moja ndani ya uwanja na hapo tena dereva akategua bomu lake. Mshambulizi alijiuwa na kusababisha nyumba zilizokuwepo karibu na uwanja huo kubomoka.
Mkuu wa polisi alisema kijiji ambako shambulio lilitokea liliwahi kuchukuliwa kama kituo cha waasi wa Taliban. Hata hivyo anasema wakazi kutokana na msaada wa maafisa wa usalama waliunda kikosi cha wanamgambo kilichowafurusha wanaharakati hao kutoka eneo hilo.