Maafisa wa masuala ya baharini wanasema maharamia wa kisomali wameteka nyara meli mbili za kigeni katika ghuba ya Aden.
Maafisa wanasema meli ya Navios Apollon iliyokuwa na bendera ya Panama, na wafanyakazi 19 ndani ilitekwa nyara jana Jumatatu ikiwa imebeba mbolea kuelekea India. Saa chache kabla, maharamia waliteka nyara meli ya St.James iliyobeba madawa ambayo ilikuwa na bendera ya Uingereza, na wafanyakazi 26. Meli hiyo ilikuwa inasafiri kutoka Spain kuelekea Thailand.
Meli hizo mbili zilikamatwa siku ambayo maharamia waliiachia huru meli ya mizigo iliyokuwa na bendera ya Singapore ya Koto Wajar, kutoka bandarini na hifadhi ya maharamia ya Haradhere, na siku moja baada ya meli ya mizigo ya China, De Xin Hai, ikiwa na mabaharia 25 iliachiwa huru.
Maafisa wa masuala ya majini wanasema meli zipatazo 10 za kigeni na zaidi ya wafanyakazi 200, hivi sasa wanashikiliwa mateka na maharamia wa kisomali. Uharamia umeongezeka kwenye pwani ya Somalia katika miaka ya karibuni.