Umoja wa Mataifa unasema uhaba wa mvua katika ukanda wa Sahel barani Afrika unamaanisha mavuno ya chakula yatapungua kwa robo tatu ya mavuno ya kawaida.
Mvua haba kutoka mwishoni mwa mwezi September hadi mwishoni mwa mwezi Octoba zimepunguza mavuno katika nchi za Niger, kaskazini mwa Nigeria, eneo la kati kati ya Chad, kaskazini-mashariki mwa Mali na Burkina Faso.
Mkurugenzi wa shirika la chakula duniani la Umoja wa Mataifa kwa ukanda wa Afrika magharibi, Thomas Yanga, anasema ongezeko la bei na utapiamlo unatarajiwa kuwa wa kiwango cha juu, na kusababisha njaa kwa baadhi ya watu. Bwana Yanga alisema idara hiyo inajiandaa kwa matatizo mapya ya ulinzi wa chakula huko mashariki mwa ukanda wa Sahel, ambapo idadi ya utapiamlo tayari imevuka kiwango cha dharura.
Mkuu wa oparesheni za WFP nchini Chad, Jean-Luc Siblot, anasema upungufu wa chakula utaongeza mara mbili tatizo la muda mrefu la utapiamlo nchini humo.