Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon amepongeza makubaliano yaliyofikiwa kati ya serekali ya Burundi na kundi la mwisho la waasi Palipehutu FNL, ambayo yatamaliza miaka 15 ya mapigano ya kikatili ya wenyewe kwa wenyewe.
Hata hivyo viongozi wa kisiasa wa kundi hilo wamesema, wamekubali kimsingi kubadili jina la kundi lenye muelekeo wa kikabila, na kiongozi wa kundi Agathon Rwasa alikiri kwamba jina halifai kutumiwa kuandikisha chama cha kisiasa.
Lakini msemaji wake Pasteur Habimana, ameiambia Sauti ya Amerika kwamba, mkataba ulotiwa sahihi wakati wa mkutano pamoja na viongozi kadhaa wa kiafrika, wakiongozwa na Rais Yoweri Museveni wa Uganda, mwenyekiti wa mazungumzo ya Burundi, walimruhusu kiongozi wao kufikisha suala hilo kwa wanachama kuamua.
Habimana alisema wamekubali kulivunja tawi lake la kijeshi na kuwakusanya pamoja wapiganaji wake katika makambi yatakayokubalika na serekali.
Kwa upande wake serikali nayo imesema itawaachilia huru waasi wote waliofungwa na kuwapa viongozi wa kundi hilo nyadhifa za serikali.