Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Septemba 18, 2024 Local time: 12:23

Upinzani Senegal unalaani uamuzi wa kucheleweshwa uchaguzi wa rais hadi Desemba 15


Polisi wavambia bunge la Senegal na kuwaondoa wabunge wa upinzani.
please wait

No media source currently available

0:00 0:00:20 0:00

Polisi wavamia bunge la Senegal na kuwaondoa wabunge wa upinzani.

Upinzani Senegal umelaani uamuzi wa bunge kuahirisha uchaguzi wa rais kwa miezi 10 na kueleza kitendo hicho kuwa ni "mapinduzi ya kikatiba,"ambacho wachambuzi wanasema kinalitumbukiza taifa hilo la Afrika Magharibi katika mzozo wake mbaya kabisa wa kisiasa katika muda wa miongo kadhaa.

Wabunge walio wengi wa chama tawala walipitisha hoja ya kuahirisha uchaguzi wa rais hadi Desemba 15 baada ya mjadala mkali na mvutano na kusukumana Jumatatu hadi wakati mmoja polisi walilazimika kuvamia kikao chao na kuwaondoa baadhi ya wabunge wa upinzani.

Hatimaye, kwa karibu sauti moja wabunge waliidhinisha mabadiliko hayo yanayomruhusu Rais Macky sall ambaye muhula wake wa pili unatarajiwa kumalizika mapema mwezi Aprili, kubaki madarakani hadi pale atakayechukua nafasi yake kuapishwa, pengine mapema 2025.

Rais Macky Sall wa Senegal akizungumza kwenye mkutano wa COP28.
Rais Macky Sall wa Senegal akizungumza kwenye mkutano wa COP28.

Babacar Abba Mbaye mbunge wa upinzani anasema hakuna neno kwenye kamusi linaloweza kutafsiri hatua yao, isipokuwa ni neno la kuongeza muda wa muhula wa rais.

“Walipotoa hati ya hoja walituambia uchaguzi unaahirishwa hadi Agosti 25. Polisi walivamia na kutuondoa ili waweze kupitisha mabadiliko hayo ya katiba. Sasa uchaguzi unafanyika Desemba 15. Kwa hivyo hivi sasa tuko chini ya utawala wa kimabavu wa mwaka mmoja wa rais Macky Sall. Tunatoa wito kwa wananchi kujitokeza na kuonyesha wakati umefika wa kutetea demokrasia.

Mtaalamu wa masuala ya katiba nchini Senegal Profesa Babacar Gueye anakosowa uwamuzi huo akilieleza shirika la habari la AFP kwamba ni ukiukaji wa misingi ya kidemokrasia na ni tukio la hatari sana ambalo halijawahi kutokea nchini humo.

"Kilichotokea jana ni tukio la kipekee la hatari, na hatari sana kwa demokrasia. Kesho rais anaweza kusimama, siku ya mkesha wa uchaguzi Desemba 15, na kurudia kitendo hicho hicho, na kubuni mazingira sawa na kusema kuna hatari ya kuzuka vurugu baada ya uchaguzi wa rais kuahirishwa tena kwa muda usojulikana."

Gueye anasema hawatakubali nchi yao ambayo imetajwa kama kitovu cha demokrasia Afrika itumbukie kwenye utawala wa kimabavu.

Wabunge kutoka chama cha Rais Sall ambao wameshindwa kukubaliana juu ya mgombea kiti cha rais aliyechaguliwa na rais mwenyewe, waliamua kuunga mkono pendekezo hilo. Mbunge wa Moussa Diakate mwenyekiti wa kamati ya sheria inayounga mkono serikali anasema, Rais Sall alisema atatumikia muhula miwili na ameshikilia ahadi yake hii si njama ya kutaka kubaki madarakani.

Muandamanaji akionesha alama ya ushindi kupinga kubadili tarehe ya uchaguzi wa rais Senegal
Muandamanaji akionesha alama ya ushindi kupinga kubadili tarehe ya uchaguzi wa rais Senegal

Ghasia zimetokea nje ya bunge tangu Jumatatu lakini inaripotiwa kwamba siku ya Jumanne hali imekua ni tulivu kukiwepo na idadi kubwa ya polisi wa kupambana na ghasia katika njia kuelekea bungeni ili kuzuia maandamano au ghasia.

Wagombea wawili wa upinzani wa kiti cha rais akiwemo waziri mkuu wa zamani Bi Aminata Toure, walikamatwa na baadaye kuachiliwa kufuatia ghasia zilizozuka mwishoni mwa wiki kupinga kuahirishwa kwa siku ya uchaguzi.

Senegal haijapata kushuhudia mapinduzi tangu kunyakua uhuru wake kutoka Ufaransa 1960.

Forum

XS
SM
MD
LG