Waziri Mkuu wa Sweden leo Ijumaa alilaani kundi la Kikurdi mjini Stockholm kwa kuning'iniza sanamu ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ikimuonesha akining'inia kwa miguu yake kwa kamba.
Utekelezaji wa "aina ya mauaji ya kejeli ya kiongozi wa kigeni aliyechaguliwa kidemokrasia" ulikuwa "mbaya sana", Ulf Kristersson aliiambia televisheni ya TV4.
Uturuki ilimuita balozi wa Sweden mjini Ankara siku ya Alhamisi baada ya Kamati ya Kikurdi ya Rojava ya Sweden kumlinganisha Erdogan na dikteta wa Italia marehemu Benito Mussolini.
Mtawala huyo wa Kifashisti alining'inizwa juu-chini baada ya kunyongwa katika siku za mwisho za vita kuu vya pili vya dunia.
"Historia inaonyesha jinsi madikteta wanavyoishia," kundi hilo liliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter, likiambatana na video inayoonyesha picha za mauaji ya Mussolini mwaka 1945 na kisha sanamu iliyochorwa kuonekana kama Erdogan akizunguka kwa kamba nje ya ukumbi wa City Hall mjini Stockholm.
Kristersson amesema kitendo hicho ni kibaya zaidi ikizingatiwa kuwa Sweden imeshuhudia wanasiasa wake wawili wakuu wakiuawa.