Chama cha Ennahdha nchini Tunisia chenye msukumo wa kiislam kiliwataka wafuasi wake siku ya Alhamis kususia kura ya maoni ya Julai 25 kuhusu katiba mpya ya Rais Kais Saied kikisema itasababisha utawala kandamizi na wa kimabavu.
Tunatoa wito wa kususia kura ya maoni kwa sababu kinachopigiwa kura si kwa maslahi ya wa-Tunisia msemaji wa chama hicho Imed Khemeri alisema katika mkutano na waandishi wa habari mjini Tunis.
Rais Saied hapo Julai mwaka 2021 aliifuta serikali na kulisimamisha bunge lililotawaliwa na Ennahdha. Baadae alipanua mamlaka yake katika kile ambacho wakosoaji wanaona kama mapinduzi dhidi ya demokrasia mahala ambapo vuguvugu la Arab Spring limeanzia.
Katiba ni kiini cha msukumo wa Saied kurekebisha mfumo wa kisiasa wa Tunisia ulizua ukosoaji wa papo hapo kwa mamlaka yasiyo na kikomo ambayo inampatia Rais.