Umoja wa Mataifa ulionya Jumatano kwamba dunia inashindwa katika juhudi zake za kutokomeza njaa kwani zaidi ya watu milioni 828 walikuwa na uhaba wa chakula hapo mwaka 2021 ikiwa ni milioni 150 zaidi ya kabla ya janga la COVID-19 hapo mwaka 2019.
Ripoti ya hali ya usalama wa chakula na lishe iliyotolewa Jumatano ni ushirikiano wa pamoja kati ya mashirika matano ya Umoja wa Mataifa ikiwemo shirika la chakula na kilimo na Program ya chakula duniani. Takwimu zao zinaonyesha kwamba vichochezi vikuu vya uhaba wa chakula na utapiamlo ni migogoro, mabadiliko ya hali ya hewa na majanga ya kiuchumi, pamoja na kuongezeka kwa ukosefu wa usawa.
Takribani watu bilioni 2.3 walikosa kupata chakula cha kutosha mwaka 2021. Kikanda, njaa iliendelea kuongezeka barani Afrika ambapo watu milioni 278 waliathiriwa, huko Asia mahala ambapo watu milioni 425 walishuhudia hali hiyo, na huko Latin Amerika na Caribbean mahala ambapo watu milioni 56.5 waliathiriwa.