Maafisa wa Ukraine siku ya jumatano waliwaambia wakaazi waliobaki huko mashariki mwa jimbo la Donetsk kukimbilia maeneo salama wakati Russia ilipoanzisha mashambulizi mapya katika jaribio la kuchukua udhibiti kamili wa eneo lenye viwanda la Donbas.
Msimamizi wa kijeshi wa jimbo la Donetsk Pavlo Kyrylenko aliviambia vyombo vya habari vya Ukraine kwamba Russia imegeuza jimbo lote la Donetsk kuwa eneo la mapigano ambapo ni hatari kubaki kwa raia.
Russia tayari inadhibiti asilimia 55 ya jimbo la Donetsk baada ya kusema kwamba katika siku za karibuni ilikuwa imechukua kabisa mkoa jirani wa Luhansk.
Rais wa Russia Vladmir Putin amesema moja ya malengo makuu ya uvamizi wake wa miezi mine na nusu nchini Ukraine ni udhibiti kamili wa sekta ya mashariki mwa jimbo la Donbas linalozungumza ki-Russia linalozunguka majimbo hayo mawili.
Baadhi ya wa-Ukraine wanapinga kuondoka Donetsk lakini Kyrylenko alisema ni takribani watu 340,000 pekee waliobaki nje ya idadi ya watu kabla ya vita iliyoathiri karibu watu milioni 1.7