Wahamiaji 22 raia wa Mali walikufa katika maafa ya boti kwenye pwani ya Libya, Umoja wa Mataifa ulisema Jumanne ukiwanukuu manusura ambao waliripoti waathirika kuzama na kuishiwa na maji mwilini na watoto watatu waliripotiwa kuwa miongoni mwa waliokufa.
Baada ya siku tisa za kuwepo baharini manusura 61 wengi wao kutoka Mali waliokolewa na walinzi wa pwani ya Libya na kurudishwa ufukweni, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wahamiaji (IOM) lilisema huku idadi hiyo ikithibitishwa na wizara inayohusika na wahamiaji nchini Mali.
Wahamiaji hao walipanda kutoka mji wa Zuwara huko Libya karibu na mpaka wa Tunisia kwa boti ya kujaza kwa upepo mwendo wa saa saba usiku kwa saa za huko hapo Juni 22 alisema msemaji wa IOM, Safa Msehli.
Msehli alisema baadhi ya wahamiaji hao walikuwa na hali mbaya kiafya na hivyo walipelekwa hospitali na IOM. Walirudishwa ufukweni siku ya Jumamosi. Libya imekuwa njia kuu ya uhamiaji usio wa kawaida barani Ulaya katika miaka ya karibuni ya machafuko tangu kupinduliwa na kuuawa kwa diktekta Moamer Gadhafi mwaka 2011 katika uasi ulioungwa mkono na NATO.