Serikali ya China inafanya kazi kuzuia kuendelea mivutano ya kidiplomasia na kulinda picha yake barani Afrika baada ya video za ubaguzi wa rangi za watoto wa kiafrika zilizotengenezwa na raia wa China anayeishi nchini Malawi kuonekana mapema wiki hii.
Ripoti ya uchunguzi ya BBC kuhusu video hizo ilimuonyesha mwanamme anayeitwa Lu Ke ambaye anadaiwa kuwarekodi watoto wa kiafrika bila wao kujua akisema maneno machafu kwa lugha ya Mandarin kama vile “mimi ni jini mweusi na sina akili nzuri”.
Video hizo kisha ziliuzwa kwenye tovuti ya China kulingana na BBC. Habari hizo zilizusha ghadhabu nchini Malawi huku wanamtandao wakielezea kukasirishwa kwao kwenye Twitter na waziri wa mambo ya nje wa Malawi Nancy Tembo anasema nchi yake imesikitishwa, kuchukizwa, kudharauliwa, na kuumizwa sana.
Baada ya ubalozi wa China nchini Malawi kukosolewa kwa majibu yake ya awali ambayo hayakuwa makali kwa kashfa hiyo na kuzipuuza video hizo kama habari za zamani kwa sababu zilirekodiwa mwaka 2020. Lakini ubalozi huo hatimaye ulitoa taarifa mpya na yenye nguvu siku ya Alhamis.