Msaidizi wa Katibu Mkuu Martha Pobee aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba uamuzi wa wiki hii wa serikali ya kijeshi ya Mali wa kuondoka kwenye kikosi hicho kwa hakika ni hatua ya kurudi nyuma kwa Sahel.
Kikosi cha G5 Sahel kiliundwa mwaka 2014 na Mali na kujumuisha mataifa jirani ya Afrika Magharibi ya Niger, Mauritania, Burkina Faso na Chad ili kukabiliana na ugaidi katika eneo la Sahel, lakini tangu mwanzo kiligubikwa na matatizo ya kifedha na kisiasa na hakikufanya kazi. Na hakikupeleka wanajeshi hadi mwaka 2017.
Hata hivyo, Pobee alisema kuwa tangu Novemba mwaka jana kikosi hicho kimefanya operesheni katika sekta zake zote tatu bila ushiriki wa vikosi vya Mali.