Nchi ya Mali ilisema Jumapili kwamba inajiondoa kutoka kwenye kikosi cha Afrika magharibi kinachopigana na wanajihadi kupinga kukataliwa kwake kama mkuu wa kundi la kikanda la G5 ambalo pia linajumuisha Mauritania, Chad, Burkina Faso na Niger.
Serikali ya Mali inaamua kujiondoa kutoka kwa vyombo na makundi yote ya G5 sahel ikiwemo jeshi la pamoja la kupambana na wanajihadi ilisema taarifa. G5 Sahel iliundwa mwaka 2014 na kikosi chake cha kupambana na jihadi kilizinduliwa mwaka 2017.
Kongamano la wakuu wa nchi za G5 Sahel lililopangwa kufanyika Februari mwaka 2022 mjini Bamako lilitarajiwa kuadhimisha mwanzo wa urais wa Mali wa G5. Lakini takribani miezi mine baada ya mamlaka kuashiria hivyo mkutano huu bado haujafanyika ilisema taarifa hiyo. Bamako inapinga vikali hoja ya nchi wanachama wa G5 ambayo inaendeleza hali ya ndani ya kisiasa kuukataa urais wa Mali wa G5 Sahel ilisema taarifa hiyo bila kuitaja nchi yeyote.