Kampuni kubwa ya mtandaoni ya Google imetangaza mwezi huu itafungua kituo chake cha kwanza cha kutengeneza bidhaa barani Afrika kitakachokuwa na makao yake katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi. Kampuni hiyo yenye makao yake mjini Mountain View California, nchini Marekani inapanga kuwekeza dola bilioni moja mnamo miaka mitano ijayo ili kulenga soko la mtandaoni linalokuwa kwa kasi katika bara hilo.
Google inataka kupata sehemu kubwa zaidi kwenye soko linalopanuka la watu wanaotumia mtandao barani Afrika ambao wanatarajia kufikia milioni 800 ifikapo mwaka 2030.
Kampuni hiyo inaanzisha kituo chake cha kutengeneza bidhaa jijini Nairobi ambacho kimepangwa kufunguliwa mwaka 2023 na kitaajiri zaidi ya watu 100.
Charles Murito ni mkuu wa masuala ya serikali na sera za umma kwa ajili ya nchi za Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara katika Google. Anasema uwekezaji huo utaunda fursa nyingi ndani ya sekta ya teknolojia ya Afrika.
“Kituo cha kutengeneza bidhaa kitakuwa kile kitakachofanya kazi kubuni bidhaa za kuleta mabadiliko na huduma kwa watu hapa barani pamoja na kutenegeneza bidhaa kwa dunia nzima. Kwa hivyo basi tangazo la wiki iliyopita lilikuwa mwanzo tu katika utaratibu wa kuajiri watu ambao watafanya kazi katika kituo hiki cha kutengeneza bidhaa Afrika. Na hiyo itajumuisha majukumu kama vile wasimamizi wa bidhaa, wabunifu na watafiti wa UX, na wahandisi, na huu ni mwanzo wa kazi ambazo tutakuwa tukiifanya”.
Kampuni hiyo ya teknolojia ya kimataifa ilisema malengo yake ni kufanya habari za ulimwengu zipatikane na watu wote na kubuni bidhaa ambazo zinafanya kazi vyema kwa wa-Afrika. Bitange Ndemo ni katibu mkuu wa zamani wa wizara ya habari, mawasiliano na teknolojia nchini Kenya. Anasema serikali inahitaji kutoa mafunzo kwa vijana wake wengi ili kufaidika na kituo cha Google.
“Ni uwekezaji mzuri kwa maana ya kwamba utasaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira katika nchi hii, lakini kile ambacho jambo hili linaieleza serikali ya Kenya , ni kwamba lazima waanze kuwekeza katika kuwapatia ujuzi vijana mara kwa mara ili waweze kukidhi mahitaji. Tayari mahitaji ya ujuzi kama huo yanazidi mahitaji ya ndani ya nchi”.
Google imetoa mafunzo kwa zaidi ya mafundi 80,000 walioidhinishwa kutoka Afrika katika miaka michache iliyopita. Kampuni hiyo inawekeza dola bilioni moja katika miradi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo kusaidia maendeleo ya uchumi wa mtandao wa Afrika.
Wakati huo huo Microsoft pia imewekeza nchini Kenya ikiajiri mamia ya wahandisi kutoka taifa hilo la Afrika mashariki.
Bara la Afrika lina changamoto zake kwa wafanyabiashara kwa sababu baadhi ya nchi hazina utawala bora na utawala wa sheria na hiyo inaweka mazingira yasiyo mazuri ya uwekezaji.
Baadhi ya mataifa yamefunga huduma ya mitandao ili kuwanyamazisha raia wao. Murito anasema shirika lake linafanya kazi na serikali za Afrika kuhimiza uvumbuzi na kuendeleza sera ambazo zitaendelea uvumbuzi.