Serikali ya Somalia na kampuni moja ya Marekani wako kwenye mzozo kuhusu uhalali wa makubaliano ya utafutaji mafuta yaliyofikiwa mwezi Februari mjini Istanbul.
Abdirashid Mohamed Ahmed, waziri wa petrol na rasilimali za madini wa Somalia na Richard Anderson, afisa mkuu mtendaji wa Coastline Exploration Ltd, walitia saini makubaliano hayo. Lakini katika taarifa tofauti, Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed anayejulikana pia kama Farmaajo, na waziri mkuu Hussein Roble waliukataa mkataba huo na kuutangaza ni batili.
Viongozi wote wawili walieleza amri ya kiutendaji ya serikali kupiga marufuku wizara zote na mashirika ya serikali kutia saini mikataba na serikali za nje pamoja na taasisi za nje hadi uchaguzi wa bunge unaoendelea utakapokamilika. Uchaguzi huo unatarajiwa kukamilika mwezi ujao kwa kuchaguliwa Rais mpya.
Aidha serikali imemuagiza mwanasheria mkuu wa serikali, Suleimani Mohamed Mohamud, ku-uchunguza mkataba huo na kuchukua hatua stahiki za kisheria.