Marekani siku ya Jumanne ilisisitiza kuunga mkono mpango wa Morocco wa kujitawala kwa Sahara magharibi ili kusuluhisha mzozo wa miongo kadhaa wa ufalme huo na vuguvugu la kudai uhuru la Polisario.
Tunaendelea kuutazama mpango wa kujitawala wa Morocco kama mzito, wa kuaminika na wa kweli, naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani Wendy Sherman alisema wakati wa ziara yake kwa mshirika wa Marekani.
Ziara yake ya kikanda pia itajumuisha mpinzani mkuu wa Morocco, Algeria. Sherman alionyesha kumuunga mkono Staffan de Mistura, mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Sahara magharibi ambaye anafanya kazi ya kufufua mchakato wa amano ambao umekwama tangu mwaka 2019.
Tunafanya hivyo kwa nia iliyo wazi kutafuta azimio ambalo litapelekea matokeo ya kudumu na yenye heshima kwa pande zote, Sherman aliwaambia waandishi wa habari baada ya kukutana na mwanadiplomasia mkuu wa Morocco, Nasser Bourita.
Bourita alibainisha msimamo wa wazi na wa mara kwa mara wa Washington kuhusu Sahara magharibi na mpango wa kujitawala.