Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 04, 2023 Local time: 16:00

Shirika la UNEP laadhimisha miaka 50 Kenya, wadau walipongeza kwa  mafanikio yake


Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akiongea katika sherehe za kuadhimisha miaka 50 ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira UNEP Gigiri, Nairobi, Kenya, Machi 3, 2022. REUTERS/Monicah Mwangi
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akiongea katika sherehe za kuadhimisha miaka 50 ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira UNEP Gigiri, Nairobi, Kenya, Machi 3, 2022. REUTERS/Monicah Mwangi

Linapoadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake jijini Nairobi, wanamazingira nchini humo wanaeleza kuwa limehamasisha na kuelimisha umma na vile vile kuichochea Kenya kubuni na kutekeleza sera muhimu na kuwa mstari wa mbele kupambana na uchafuzi wa mazingira na kukabili mabadiliko ya tabia nchi.

Tangu mwaka 1972, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira UNEP limekuwa mhamasishaji mkubwa wa masuala ya mazingira duniani.

Wakati linapoadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake jijini Nairobi, wanamazingira nchini humo wanaeleza kuwa limehamasisha na kuelimisha umma na vile vile kuichochea Kenya kubuni na kutekeleza sera muhimu na kuwa mstari wa mbele kupambana na uchafuzi wa mazingira na kukabili mabadiliko ya tabia nchi.

Muziki na tafrija imekuwa sehemu ya maadhimisho haya ya miaka hamsini tangu shirika hili la Umoja wa mataifa kuanzishwa hapa Gigiri jijini Nairobi.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, Rais wa Nigeria Muhamadu Buhari na mwenzake wa Botswana Mokgweetsi Masisi, wamewaongoza zaidi ya wajumbe 2,000 kutoka zaidi ya mataifa 170 ambao ni wakuu wa serikali, wataalam, mashirika ya kiraia, wanasayansi na sekta binafsi kuchukua hatua kuhusu masuala ya dharura ya mazingira ikiwemo mabadiliko ya hali ya hewa, upotevu wa asili na viumbe hai, uchafuzi wa mazingira na taka na kuchukua hatua bora za kutatua majanga ya sayari.

Serikali ya Kenya inaeleza kuwa maadhimisho haya yanaikumbusha dhima ya kuhimiza mazingira safi, yenye afya na kutumika kwa uendelevu kuhudumia ubinadamu.

Februari 28, 2017, serikali ya Kenya chini ya kifungu cha 3 na 86 cha Sheria ya Usimamizi na Uratibu wa Mazingira na kupitia tangazo la Gazeti la Serikali ilipiga marufuku matumizi, utengenezaji na uingizaji wa mifuko yote ya plastiki inayotumika kwa biashara na majumbani.

Utekelezaji wake, kwa mujibu wa serikali, umewezesha mafanikio ya zaidi ya asilimia 80, lakini changamoto bado zingalipo anavyoeleza Dkt Namenya Dan Naburi, mtaalam wa masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.

Katika kampeni yake iitwayo “Greening Kenya Campaign” iliyozinduliwa Desemba 2018, ambayo inaangazia kukuza miti shuleni, vyuo vikuu, vituo vya elimu, mashamba na maeneo makavu ya nchi na katika miji mikuu, Kenya imedhamiria kupanda miti bilioni 1.8 na kufikia zaidi ya asilimia 10 ya kiwango cha misitu ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Licha ya Kenya kukabiliwa na changamoto nyingi za mazingira ambazo ni pamoja na ukataji miti, mmomonyoko wa udongo, uharibifu wa ardhi, kuenea kwa jangwa, kupotea kwa viumbe hai, uhaba wa maji na uchafuzi wa mazingira kutoka viwandani, serikali ya rais Uhuru Kenyatta inaeleza kuwa kupiga marufuku matumizi, utengenezaji na uingizaji wa mifuko ya plastiki, ni mapambano makubwa zaidi katika vita dhidi ya uchafuzi wa mazingira.

Mwanamazingira Elizabeth Wathuti ameeleza kuwa hayo hayatoshi na panastahili kuwapo juhudi pana za kukabili mabadiliko ya tabia nchi na Kenya kama mwenyeji wa shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, linastahili kujitahidi zaidi.

Kenya ni mojawapo wa nchi za kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki kupiga marufuku matumizi ya plastiki na kutia saini mpango wa Bahari Safi wa kuondoa taka za plastiki kwenye chemchemi za maji.

Tangu Juni 2020, Kenya iliwazuia wageni wanaotembelea mbuga za kitaifa, ufuo, misitu na hifadhi nyingine hawawezi tena kubeba chupa za plastiki za maji, vikombe, sahani zinazotupwa baada ya kutumika au mirija inayotumika kunywa maziwa au soda.

Watalaam wa mazingira wanasisitiza kuwa serikali inastahili kuongeza nguvu kukabili vichafuzi vya mazingira, kubuni sera zinazoweza kuongeza uendelevu wa kuimarisha ukuaji wa uchumi, kubuni nafasi za kazi na kuwaondoa watu kutoka kwenye umaskini.

Rais Uhuru Kenyatta Alhamisi ametangaza kwamba serikali yake itadhamini tuzo ya $20,000 kuwatambua watetezi wa mazingira na amani, na kutolewa mara mbili kwa mwaka kwa watu na taasisi zinazosimamia njia bunifu zkutunza mazingira.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Kennedy Wandera Nairobi, Kenya

XS
SM
MD
LG