Sudan imemsamahe na kumuachia huru kiongozi wa kundi la wanamgambo wa Janjaweed Musa Hilal, aliyewekewa vikwazo na umoja wa mataifa na kushtumiwa na makundi ya haki za binadamu kufanya ukatili katika jimbo la Darfur, mshauri wake amesema jana.
Kuachiliwa kwa Hilal na wanachama wengine wa kundi lake kunajiri wakati serekali ya mpito ya Sudan inaendeleza juhudi za amani katika kanda ya magharibi iliokumbwa na vita, kufuatia mkataba wa amani wa mwezi Oktoba na makundi ya waasi ambao umelenga kumaliza mzozo wa miongo kadhaa.
“Musa Hilal ameachiliwa pamoja na wenzake”, mshauri wa karibu wa Hilal, Ismail Aghbash ameliambia shirika la Habari la AFP.
Hilal alikua anazuiliwa tangu mwaka wa 2017.
Hilal alikua mtu wa karibu sana rais aliyeondolewa madarakani Omar al Bashir, ambae aliunga mkono wapiganaji wa kiarabu wa kundi la Janjaweed dhidi ya makabila ya kiafrika ya wachache waliotengwa, wakati vita vilizuka Darfur mwaka wa 2003.
Mapigano ambayo yalipungua miaka ya hivi karibuni, yaliuwa watu laki 3 na kuwaondoa katika makazi yao wengine millioni 2 na laki 5, kwa mujibu wa umoja wa mataifa.
Hilal aliwekewa vikwazo na umoja wa matifa mwaka wa 2006 kwa madai ya kusimamia ukatili Darfur, umoja wa mataifa ukimshtumu kukiuka sheria ya kimataifa ya wakati wa vita Pamoja na sheria ya haki za binadamu.